HISTORIA ya udhalimu, vitisho na mauaji ya kinyama yamerekodiwa kwenye nyaraka mbalimbali ndani na nje ya Tanzania kwa nyakati tofauti. Udhalimu, vitisho na mauaji ya kisiasa yamekuwa mambo yenye laana! Hata hivyo vitendo hivyo vilivyorekodiwa kwenye kumbukumbu za harakati za kisiasa, kiuchumi na kijamii vinahusisha taasisi nyeti zilizoundwa kwa mikakati maalumu kunyamazisha sauti ya upinzani juu ya uhuru na haki ya watu katika jamii.
Udhalimu ni tabia ya kishenzi. Udhalimu unahusisha kufanya mambo yaliyo kinyume na haki, uonevu, hiana na ukatili (tazama Kamusi ya Kiswahili Sanifu – TUKI, ukurasa 423 toleo la 2008).
Udhalimu mara zote hufanywa na watu wenye chuki, roho mbaya na tabia za kishenzi na au zisizokuwa na chembe ya ucha Mungu kwa maslahi binafsi na au ya kimfumo katika kulinda na kutetea masilahi ya kifisadi na au kifasiki.
Hivi ndivyo ilivyo, wenye satwa (nguvu) na mamlaka kwenye msonge wa utawala wa siasa, uchumi au jamii kuweka “vikosi maalum na vya siri” vya kidhalimu katika kulinda utawala na watawala.
Makala hii imekuja baada ya tafakari ya vitendo vya kidhalimu, vitisho na mauwaji vinavyoendelea duniani na Tanzania kadhalika! Inawezekana msomaji ukajiuliza masuala mengi juu ya ukweli na uhakika kwamba: Je, Tanzania kuna udhalimu, vitisho na mauwaji yasiyozingatia uhuru na haki? Jibu la haraka linaweza kuwa hapana! Kinyume chake; Tanzania ina aina zote za udhalimu, utesaji, vitisho na hata mauwaji ya watu kwa misingi inayokwenda kinyume cha haki za binadamu. Tofauti ni moja: upeo wa vitendo vya kidhalimu, utesaji, vitisho na mauaji. Tanzania haiwezi kuwa “kisiwa cha amani” kwa vile udhalimu, utesaji na mauaji yangalimo!
Vitendo hivi hufanywa kwa mfumo wa kitaasisi. Zipo taasisi zilizoundwa na mamlaka za nchi (dola) na zipo zilizoundwa na magenge ya kijambazi yanayomiliki nguvu kubwa ya fedha na mtandao kama vile “Genge la Mafia” na magenge mengine yanayoratibu biashara ya dawa za kulevya.
Utendaji kazi wa taasisi hizi unafanana sana kwa vile zote zinatumia mifumo inayofanana. Mikakati na mbinu zinazotumika ni pamoja na: kukamata watu (wahanga) kwa kuwateka nyara; kuwaweka chini ya ulinzi (isivyo halali); kuwatesa kikatili (na kinyama); kuwatisha (kuwaogofya); na hata kuwaua na kupoteza ushahidi. Kwa ujumla, taasisi zinazohusika na udhalimu wa aina hii hufanyakazi kwa usaidizi wa mfumo wa kitaasisi wenye matumizi makubwa ya hila, mizengwe na mizungu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Mfumo wa polisi wa kisisasa unaotumika na serikali nyingi duniani ni ule wa kuajiri watu maalumu kwenye kundi maalumu linaloitwa polisi wa siri (secret police) wanaopewa mafunzo maalumu katika utesaji na uuaji katika mazingira yanayoficha ukweli.
Kazi ya polisi wa siri hufanywa kwa mazingira ya “usiri mkubwa” na kwa utumizi wa nguvu kubwa ya kimamlaka. Miongoni mwa tabia ya uanzishwaji na utendaji kazi wa taasisi zinazofanya kazi kwenye mfumo wa polisi wa kisiasa ni kuwapo kwa watumishi wanaojulikana kama mashushushu, watoa taarifa, mawakala wachochezi na wauaji. Kazi kubwa ya watu hawa ni kutafuta taarifa (data) za watu wanaowaona “tishio” kwa mifumo wanayoifanyia kazi na kuwapoteza!
Kazi kubwa ya mfumo wa polisi wa kisiasa ni kutafuta viongozi wanaopinga mifumo ya kisiasa inayotawala. Au, kuwatafuta viongozi wa migomo ya wafanyakazi, wanafunzi au wananchi na kuwaweka kwenye kilengeo cha kuwashughulikia! Wakati mwingine, kama ilivyo kwenye mifumo ya kisiasa, mawakala wachochezi (wanaofanya kazi chini ya kivuli cha polisi wa kisiasa) wanaweza kuchochea upinzani wa kisiasa kwa kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani (au uhalifu) ili kupata sababu za kuwakamata viongozi halali wa upinzani.
Hii ndio “michezo michafu” inayofanywa mara nyingi kwenye mfumo wa siasa za upinzani (rejea: Matukio ya vurugu za kisiasa Zanzibar – ambapo kinyesi kilikuwa kikimwagwa kwenye visima vya maji).
Naomba sasa tufuatane kuangalia mifano ya matumizi ya polisi wa kisiasa na matukio yaliyorekodiwa na dunia ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Tuanze na mfano wa mbali sana! Huu ni mfano maarufu na wa jinsi yake kwa vile unagusa nyanja zote za kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Yesu Kristo (Rehema na amani juu yake) alikuwa mwalimu mkuu aliyetumwa kuleta “amani” na mwongozo kwa wana wa Israeli ili wamfuate na kuokoka. Hili halikuwapendeza wana wa Israeli; wakapanga njama ya kumuua! Mpango wa kumuua Yesu Kristo ulipangwa na wakuu wa makuhani (tazama Mathayo 27: 1 – 2). Huu ni ushahidi wa wazi kwamba mipango ya udhalimu na utesaji hata mauaji hupangwa na “wakubwa” kwenye mfumo wa kisiasa, kijamii au kiuchumi!
Mfano mwingine ni njama za kumuua Mtume Muhammad (SAW). Mpango ulipangwa baada ya mateso mengi yaliyowakuta wafuasi wake kama vile Bilal bin Rabah (aliyekuwa na asili ya Uhabeshi – Ethiopia/Elitrea). Pamoja na njama za kumuua kushindwa mara kadhaa alipewa mateso ya kiakili na kimwili hata wakati mmoja alipigwa mawe na kung’olewa meno ya mbele!
Yote ya udhalimu na mateso yalipangwa na kuratibiwa na wakubwa wa makafiri wa Kikureshi (waliyekuwa wakimuona kiongozi huyo wa kiroho kama tishio kwenye utawala wao wa kishenzi). Udhalimu na utesaji kama sehemu ya kuwanyamazisha wapinzani uliendelezwa katika tawala na mamlaka tofauti kwa karne nyingi sana.
Mfano wa kutisha wa zamani na unaohadithiwa sana katika jamii ya kidini katika maedhehebu ya Shia (Ithnaasharia na baadhi ya madhehebu ya Sunni) ni kuuawa kikatili kwa Imam Hussayn (AS) aliyekuwa mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW). Hussayn bin Ali (AS) aliupinga utawala wa Yazid bin Muawiya aliyekuwa akitawala kutoka Sham (Dameski au Damascus – Syria ya sasa) baada ya Muawiya bin Sufian kumtawalisha mwanawe (Yazid). Yazid, kama mtawala, aliamua kumtafuta Imam Hussayn (AS) kwa njia zote zikiwamo za kumvizia ili kumuua!
Historia inaonyesha kwamba Yazid alifanikiwa kummaliza Imam Hussayn (AS) katika eneo la Karbala (Iraq) kwa kumuua pamoja na wafuasi wake 72. Kikubwa kinachoweza kukumbukwa kwenye tukio hili la Karbala ni kule kwa Imam Hussayn (AS) na wafuasi wake kuzingirwa na majeshi ya Yazid, kunyimwa fursa ya maji ya kunywa, na baadaye kumuua Imam Hussayn (AS). Kichwa cha Imam Hussayn (AS) kilikatwa na kupelekwa kwa Yazid, mjini Dameski (Syria)! Msomaji unaweza kushangaa; usishangae hivi ndivyo wafanyavyo wenye mamlaka na wenye nguvu za kijeshi na maamiri jeshi wakuu! Wanapenda kukubali laana ya damu ya wahanga iwamwagikie kwenye mikono yao huku wakichekelea kana kwamba wataishi milele – ni washenzi na waliolaaniwa, siyo?!
Mfano mwingine ni udhalimu, mateso na mauaji aliyofanyiwa Patrice Lumumba! Siku ya uhuru wa Kongo ya Kinshasa (leo inaitwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC) Patrice Lumumba alitoa “hotuba” iliyoonyesha ‘ushenzi’ wa Wabelgiji (Wabelgiji) walioufanya kwa wananchi wa Kongo na kuahidi kuwapa wananchi wa Kongo uhuru na haki yao waliyoporwa na Wabelgiji.
Wabelgiji hawakufurahishwa na maneno ya Lumumba; walishirikiana na Marekani kuanzisha hamkani ya kisiasa na hatimaye kumpoteza mwanamapinduzi wa Afrika! Lumumba, akiwa Waziri Mkuu wa Kongo, alihuzurishwa na Rais Joseph Kasavubu aliyetumwa na mabwana wakubwa (Wabelgiji na Marekani) baada ya Jimbo la Katanga kutangaza kujitenga. Patrice Lumumba alikamatwa na askari wa jeshi la Kongo wakiongozwa na Joseph Mobutu Sese Seko.
Lumumba alichukuliwa kutoka Kinshasa kwa ndege huku akiwa amefungwa kamba mikono nyuma na kupelekwa Katanga. Katika mahojiano yaliyofanywa kwenye kumbukumbu ya mauaji ya Patrice Lumumba, kiongozi wa polisi wa Katanga (Mbelgiji) alikiri kwamba Lumumba alifikishwa kwenye eneo alilouawa akiwa na wenzake wawili! Lumumba na wenzake waliteswa sana; kisha walipigwa risasi kwa zamu na miili yao kukatwakatwa (kama nyama). Vipande vya miili yao viliyeyushwa kwenye tindikali (concentrated acid) na vingine vilichomwa moto! Masimulizi haya yaliyofupishwa (sana) yanaonyesha muhtasari wa mateso makali na ya kutisha aliyoyapata Patrice Lumumba hadi kufa tarehe 17 Januari, 1961. Hata leo hakuna anayejua (isipokuwa waliyemtesa na kumuua) jinsi alivyoteswa na kuuawa kinyama.
Msururu wa watu maarufu waliouawa na polisi wa kisiasa ni mrefu. Vilevile, kuna watu waliyepotea na hadi leo hawajulikani walipo na au hata mahali walipozikwa! Wakati mwingine wahanga walikuwa wakipotea kwa kulazimishwa (forced disappearance).
Kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, kupotea kwa kulazimishwa kunatokea wakati mtu anapokamatwa kwa siri na kufungwa na serikali au na mtu kwa amri (mamlaka), usaidizi (msaada), au kwa ridhaa ya serikali (dola), na kufuatiwa na kukanusha kujua au kutoa taarifa za aliyepotea ili kumfanya mhanga huyo kuwa nje ya ulinzi wa sheria (rejea Henckaerts, J na Louise Doswald-Beck (2005), International Committee of the Red Cross [ICRC], Cambridge University Press, ukurasa wa 342).
Waliopotea na au kuuawa katika Afrika pamoja na Patrice Lumumba ni: Felix Moumie wa Kameruni aliyeuawa kwa sumu mwaka 1960; Sylvanus Olympio wa Togo aliyepotezwa mwaka 1963; Mehd Ben Barka kiongozi wa upinzani wa Morocco alitekwa Ufaransa na mwili wake haukuweza kuonekana hadi leo.
Ukiachilia mbali mifano hiyo iliyochorwa kutoka katika sehemu tofauti za dunia kwa msisitizo wa aidha kufanyiwa udhalimu, utesaji au mauaji; turudi eneo letu la Afrika ya Mashariki. Tuanze na jirani zetu Kenya ambapo matukio ya kupotezwa (kwa kuuawa) yamerekodiwa kwenye historia ya nchi hiyo na dunia kadhalika. Mauaji ya Tom Mboya na Robert Ouko ni mifano ya moja kwa moja ya ushiriki wa “polisi wa kisiasa” wanaotumika na viongozi watawala na wenye mamlaka kuwanyamazishwa wapinzani wa kisiasa!
Uganda ya ‘dikteta’ Iddi Amin Dada ilishuhudia hali ya kupotea kwa na au vifo vya watu katika mazingira ya kutatanisha na yasiyoelezeka. Wengi wa wale waliyekuwa wakionekana wakipinga utawala baina ya 1970 hadi 1978 walipotezwa na au kuuawa kwa njia zisizoelezeka.
Sasa tumalizie na Tanzania kwa jinsi ya kumalizia uchambuzi huu kwa mukhtadha wa hali na matukio ya zamani na hivi karibuni. Historia ya “waliyopotea” katika Tanzania haitaweza kuachwa bila ya kumtaja Abdullah Kassim Hanga na kuelezea jinsi alivyopotea! Inawezekana wasomaji wengi wasimtambue mwanasiasa huyu kwa vile historia ya Tanzania imechakachuliwa, imevurugwa sana, na ukweli mwingi umefichwa. Huu ndio ukweli juu ya Abdullah Kassim Hanga!
Abdullah Kassim Hanga ndiye aliyekuwa Makamu wa Rais wa Zanzibar baada ya mapinduzi ya Januari 12, 1964. Vilevile, Abdullah Kassim Hanga alikuwa waziri wa viwanda wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuanzia tarehe 27 Aprili, 1964.
Salim Said Salim (2009) anaandika, “Nilichofanikiwa katika utafiti wangu ni kwamba Hanga alikuwa amewekwa kizuizini katika Gereza la Ukonga, Dar es Salaam, eneo wanalokaa wafungwa waliohukumiwa kifo. Wakati nikiwa gerezani Ukonga baada ya kukataa kuwa shahidi wa kupangwa wa kesi ya mauaji ya mzee Karume, nilifanya mbinu kufika eneo hilo na kukuta mipapai aliyoipanda marehemu Hanga na watu waliokuwa wamehukumiwa kifo, walinieleza hali ilivyotokea siku Hanga alipochukuliwa kupelekwa Zanzibar. Mmoja wao aliniambia Hanga ambaye aliwabembeleza wasimpeleke Zanzibar aliwaaga wafungwa huku akitokwa machozi na kuwaaambia: ‘‘Tutaonana akhera.” Hapo Ukonga alipakiwa katika gari aina ya Land Rover kwa safari ya Zanzibar, lakini kilichotokea katika safari hiyo au alipofika Zanzibar (kama alifika) hakijulikani.”
Kwa maana hiyo ni kwamba: Abdullah Kassim Hanga aliuawa mikononi mwa vyombo vya dola (enzi za Nyerere na Karume). Haijulikani aliuawa vipi na mwili wake ulifukiwa wapi (rejea barua ya Profesa Haroub Othman aliyowaandikia Maalim Seif Sharif Hamad na Aman Abeid Karume tarehe 22 Julai, 2000 kutoka Monrovia, Liberia). Pamoja na Abdullah Kassim Hanga walipotea kina: Abdul’Azizi Twala; Mohamed Abdul Meki; Abdullah Macho; na wengine waliopotezwa na hadi leo hawajulikani walipofia na au kuzikwa!
Kwa ujumla, udhalimu, utesaji na mauaji yalifanywa sana na watawala wa Afrika ya Mashariki kwa aidha utashi wao wa kimamlaka au kwa msukumo wa mabwana wakubwa kutoka nje wenye masilahi ya kisiasa, kiuchumi au kijamii.
Wengine waliouawa katika mazingira tata ni: Dakta Nicas Mahinda aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara (awamu ya Benjamin Mkapa); Imran Kombe aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa (awamu ya Ali Hassan Mwinyi); na Horace Kolimba (aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM) aliyekufa kiaina akiwa kwenye usaili msongo (stress interview) Dodoma! Pamoja na yote ya udhalimu, utesaji na mauaji yanayosukumwa na roho mbaya, chuki na ufisadi wa kimaadili dunia imewekewa na kuzikubali sheria, kanuni na taratibu za kuhakikisha kwamba dunia inakuwa mahala salama pa kuishi! Ibara ya 13 (6) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 (2005) inasema, “ni marufuku mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinaomtweza au kumdalilisha.” Vilevile, Ibara ya 15 (2) inakataza mtu kukamatwa, kufungwa, na kuwekwa kizuizini pasipokuwa na uhalali wa kufanya hivyo.
Kama kila mtu ana haki ya kusihi (haki ya uhai) kwa mujibu wa Ibara ya 14 na kama kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru kama ilivyo kwenye Ibara ya 15 (1) inakuwaje serikali inatengeneza taasisi za serikali zinazokatisha haki hiyo ya raia kuishi kwa vile tu raia hao wanakinzana na utashi wa serikali? Je, huu ni utawala bora kwa mujibu wa sheria zilizokubaliwa? Kama si utawala wa kishenzi; huu ni nini?! Inawezekana (narudia kwa msisitizo) inawezekana wapo watawala wa dunia wanaodhani kwa kufanya udhalimu, utesaji na mauaji ya kisiasa, kijamii au kiuchumi wanaweza kuwanyamazisha wapinzani wa sera za kishenzi za kisiasa, kiuchumi na kijamii! Ukiachilia mbali laana wanayopata madhalimu, watesaji na wauaji naomba watazame mwisho wa Joseph Mobutu Sese Seko, Saddam Hussayn, Muammar Gaddafi, Hosni Mubarak na wengine wenye majina yao hapa Tanzania na kwingineko: ‘walikwina?’