HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumatano, 4 julai 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Shule kongwe kuboreshwa

JIBU LA SWALI LA MBUNGE Lushoto

na Mwandishi wetu, Dodoma

 

SERIKALI imebainisha mkakati wake wa kuboresha shule kongwe zilizoko hapa nchini kwa kupeleka shilingi milioni 50 kwa kila shule hizo ili ziweze kurudi katika hali yake ya mwanzo.

Hayo yalibainishwa bungeni jana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Elimu, Kassim Majaliwa Wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Lushoto Henry Shekifu aliyetaka kujua namna serikali inavyotekeleza sera ya ujenzi wa madarasa.

Majaliwa alisema mkakati huo una lengo ya kurudisha hadhi ya shule hizo kama ilivyokuwa awali na kutimiza nia ya serikali ya kuhakikisha shule zinaboreshwa na kupatiwa huduma inayostahili.

Aidha alifafanua kuwa halmashauri zote zilizopo nchini zitapokea fungu la shilingi milioni 24 kwa ajili ya kujenga maabara na kununua vifaa katika shule zenye mchepuo wa Sayansi.

Katika swali la msingi mbunge wa viti maalum Zaynab Vullu (CCM) alitaka kujua ni lini serikali itakamilisha ujenzi wa maabara, Maktaba na miundombinu muhimu katika shule ya Kata ya Vigwaza.

Akijibu swali Hilo Majaliwa alisema ni jukumu la serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa maendeleo kuhakikisha utoshelevu wa miundombinu na katika mwaka wa fedha wa 2012/2013 Halmashauri ya Bagamoyo imetengewa shilingi milioni 108 kwa ajili ya maabara na shilingi milioni 144 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.



juu