WIZARA ya Kilimo, Chakula na Ushirika, imejitetea na kutoa sababu za kutonunua zao la mtama na mazao mengine katika ukanda wa kati kuwa ni uchache wa mazao hayo katika maeneo husika.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Adamu Malima, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kishapu, Suleiman Nchambi (CCM), ambaye alitaka kujua ni kwa nini serikali isinunue mazao ya mtama na uwele kutoka kwa wakulima kama inavyofanya kwa mazao ya mahindi.
Suleiman pia aliihoji serikali kuwa haioni kwa kununua mazao hayo kutoka kwa wakulima kwa bei nafuu, yanaweza kuhifadhiwa na kutumika wakati wa njaa na majanga na kuifanya kuokoa fedha zake nyingi.
Malima alisema serikali imekuwa ikitenga fedha nyingi kwa ajili ya kununua mazao ya chakula kwa ajili ya akiba kupitia Wakala wa Chakula (NFRA) na ambayo hutumika kwa ajili ya kusaidia wananchi katika majanga ya njaa.
Alisema kuwa mazao ya mahindi ndiyo hununuliwa zaidi kutoka katika maeneo yanayozalisha mazao hayo lakini mtama na uwele hayanunuliwi sana kutokana na uzalishaji wake kuwa mdogo hapa nchini.
Malima aliongeza kuwa mpango wa serikali ni kupanua wigo wa mazao ya hifadhi ikiwa ni pamoja na mazao ya mtama na uwele na kwamba hivi sasa serikali inaendelea kununua zao hilo endapo itabainika kuwa litapatikana kwa wingi unaohitajika.
Alisema serikali tayari imepanua wigo wa soko la mazao kwa kuanzisha bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko ambayo itanunua pia mtama na uwele.
Kwamba serikali iko tayari kununua mtama hata katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha 2012/13 endapo itabainika kuwa mtama unapatikana kwa wingi unaotakiwa.