BONDIA mkongwe wa Tanzania, Rashidi Matumla ‘Snake Man’ leo jioni anatarajiwa kupanda ulingoni nchini Ujerumani kuwania ubingwa wa dunia unaotambuliwa na IBF, uzani wa Super Middle.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam jana, mratibu wa safari hiyo, Ally Bakari ‘Champion’ ambaye ni Mkurugenzi wa Champion Sports Promotions, alisema kuwa pambano hilo litakuwa la raundi 12.
Alisema kuwa Snake Man atacheza na bondia Benjamin Simon wa Ujerumani, ikiwa ni jitihada za mkongwe huyo kujaribu kurejesha jina na heshima yake katika ulimwengu wa masumbwi, ambapo ameahidi kufanya kila awezalo kuhakikisha analitwaa taji hilo.
“Bondia mkongwe nchini Rashidi Matumla kesho ‘leo’ atapanda ulingoni nchini Ujerumani kuwania ubingwa wa dunia wa IBF, atacheza na bondia anayeitwa Benjamin Simon wa Ujerumani,” alisema Champion.
Alisema kuwa pambano hilo la kuwania ubingwa wa dunia wa IBF, litasimamiwa na German Boxing Association na kwamba, Matumla akifanikiwa kushinda atajitengenezea nafasi nzuri ya kuwania mikanda mingine ya uzani huo.
Aidha, alisema baada ya pambano hilo, Matumla anatarajiwa kurejea nchini Jumanne Julai 17, 2012 akipitia Nairobi nchini Kenya.