WIZARA ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema kampuni ya mikopo ya nyumba ya Tanzania Mortgage Refinancing Company (TMRC) haitoi mikopo ya nyumba kwa mtu mmoja bali hutoa mikopo kwa benki zenye hisa katika kampuni hiyo.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole- Medeye alitoa kauli hiyo bungeni jana na kuongeza kuwa benki zilizonunua hisa TMRC ndizo zenye nafasi ya kukopa katika kampuni hiyo na wao ndio wanaweza kukopesha wananchi kwa ajili ya kujenga, kununua au kukarabati nyumba.
Alisema TMRC ni kampuni binafsi ambayo ilianzishwa kwa mkopo wa dola milioni 30 kutoka Benki ya Dunia, ili kufanikisha upatikanaji wa mtaji wa mikopo ya nyumba hapa nchini.
Alizitaja benki ambazo zimenunua hisa katika kampuni hiyo kuwa ni CRB, Azania Bank, TIB, Exim Bank, Dar es Salaam Community Bank, NIC Bank, Banc ABC, NBC, People Bank of Zanzibar na BoA.
Hata hivyo, alisema hadi kufikia Mei mwaka huu ni moja benki ya Azania pekee ambayo ilikuwa imejitokeza na kupewa mkopo na TMRC wenye thamani ya sh bilioni 4.2 na kwamba benki hiyo imetoa mikopo ya nyumba kwa wakopaji 95.
Naibu Waziri huyo alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu swali la msingi la mbunge wa Viti Maalum, Kidawa Hamid Saleh (CCM), aliyetaka serikali imweleze yeye pamoja na Watanzani wote mikopo ya nyumba kupitia TMRC inatolewa kwa utaratibu gani na kwamba mpaka sasa ni watu wangapi wameshapata mikopo ya nyumba kupitia utaratibu huo.