HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumamosi, 18 agosti 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Simba, Mtibwa kiama BancABC SUP8R leo


na Clescencia Tryphone

 

KITENDAWILI cha nani atakayetwaa Kombe na kitita cha sh milioni 40 kitateguliwa leo kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam, pale Simba ‘Wekundu wa Msimbazi’ watakapoumana na Wakati Miwa wa Mtibwa katika fainali ya michuano ya BancABC SUP8R.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Kitengo cha Fedha cha BancABC, Mwalimu Zuberi, alisema, kabla ya mtanange wa Simba na Mtibwa, kutakuwa na mechi ya utangulizi kati ya timu ya wafanyakazi wa benki hiyo na Gymkhana kuanzia saa 8:00 mchana.

Zuberi alisema, katika mechi hiyo, wao kama wadhamini wa michuano hiyo watatoa fulana kwa mashabiki 2,000 watakaowahi kuingia uwanjani, ambako pia kila bao litakalofungwa watalinunua kwa sh 100,000, ambako fedha hizo zitakwenda kwa kituo cha kulea watoto yatima cha Kiwohede.

Akizungumzia mtanange huo, Ofisa Habari wa Wekundu hao, Ezekiel Kamwaga alisema, wao Simba hawana shaka, licha ya kuwakilishwa na kikosi B, wamepanga kulitwaa kombe hilo na kuendeleza historia yao, ikiwa ni mwanzo wa michuano hii.

“Sisi Simba tulishazoea kila michuano yoyote inapoanza, lazima tutwae kombe tukiwa wa kwanza, kwa hiyo hata hili hatutakubali liende Mtibwa na kuharibu CV yetu,” alisema Kamwaga.

Naye, Kocha Mkuu wa Mtibwa, Mecky Mexime, aliwapongeza Yanga kwa kujitoa katika michuano hiyo na wao kuweza kupata fursa ya kushiriki, huku akikiri mchezo wa leo utakuwa mkali na mzuri, kutokana na uwezo wa kikosi cha Simba.

“Mimi nimewaangalia Simba katika mechi zao ni wazuri, hivyo basi licha ya uzuri huo sisi kesho (leo), hatutakubali kombe kwenda Msimbazi, tutapigana kufa na kupona,” alisema Mexime.

Mbali ya bingwa kuondoka na kitita cha sh milioni 40, mshindi wa pili atajinyakulia sh milioni 20, timu mbili zilizoishia nusu fainali kila moja sh milioni 15 na timu shiriki zilizobakia zitajipoza kwa sh mil 5 kila mmoja.



juu