MBIO za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2012/ 13, zimepangwa kuanza Septemba mosi, zikishindanisha jumla ya timu 14.
Kabla ya kuanza kwa ligi hiyo, baadhi ya timu zilipata nafasi ya kushiriki michuano kadhaa ambayo kwa sehemu fulani ilitumika kuvijenga vikosi vilivyosheheni nyota wa zamani na wale wapya.
Miongoni mwa timu zilizopata nafasi ya kushiriki michuano tangu kwisha kwa Ligi Kuu ya Bara Mei 6, mwaka huu ni Simba, Yanga na Azam zilizoshiriki michuano ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kagame Cup.
Ingawa ubingwa wa michuano hiyo ulikwenda kwa Yanga, bado timu za Simba iliyoishia hatua ya robo fainali katika michuano hiyo na Azam FC iliyofika hadi fainali, zilipata nafasi ya kupima uwezo wa nyota mmoja mmoja na kikosi kwa ujumla.
Kabla ya michuano hiyo ya Kagame iliyofanyika jijini Dar es Salaam, timu za Azam na Simba, zilipata fursa nyingine ya kucheza michuano mipya ya Ujirani Mwema ambayo ilichezwa Visiwani Zanzibar, ambapo ubingwa ulikwenda kwa Simba. Aidha, baada ya kwisha kwa michuano ya Kombe la Kagame, Simba, Mtibwa na Azam zikashiriki michuano maalumu ya BancABC Supe8r, ambayo pia ilitosha kuwa kipimo kwa timu hizo ingawa kwa upande wa Simba, walitoa nafasi kwa nyota wa kikosi cha pili.
Ukiondoa timu za Simba, Yanga, Azam na Mtibwa Sugar ambazo walau zimepata nafasi ya kupima nyota wao hivyo kuelekea kwenye Ligi Kuu ya Bara wakiwa na picha kamili ya uwezo wa vikosi vyao, nyingine zilikosa fursa hiyo.
Sisi Tanzania Daima ambao ni sehemu ya wadau wa michezo na maendeleo kwa ujumla wake, tunaona haja ya kuzikumbusha timu zote za Ligi Kuu, kutumia vizuri kipindi hiki kifupi kilichobaki kabla ya kuanza kwa ligi hiyo kunoa vikosi.
Tunasema hili kwa kuzingatia kuwa, kama timu zote 14 zitakuwa kwenye kiwango bora kiuchezaji, tunaamini ndio ufanisi wa ligi yenyewe kwani itakuwa na ushindani unaotarajiwa dimbani badala ya kushuhudia timu moja ikiwa kibonde dhidi ya nyingine.
Ushindani mzuri ni pamoja na timu kupata ushindi dhidi ya timu bora, si kupata ushindi dhidi ya timu kibonde kwani ushindi wa aina hiyo, huwa hauna maana yoyote kama kweli tunataka kupata bingwa bora wa kutuwakilisha vema kwenye michuano ya kimataifa.
Kwa mantiki hiyo, ni wajibu wa timu nyingine pia kuona umuhimu wa kujifua sasa ili kuwa shindani katika ligi hiyo badala ya kuishia kugawa pointi kwa timu nyingine zilizoonekana walau kujiandaa vizuri kama Simba, Yanga, Azam na Mtibwa Sugar.
Tungependa kuona ligi hiyo haiwi ya timu hizo tu, bali timu zote kucheza soka maridadi ili kuondoa ukiritimba wa Simba na Yanga katika soka yetu, kwani hilo nalo limechangia kwa kiasi kikubwa kudumaza soka yetu na ndiyo maana tumekuwa tukipongeza ujio wa Azam.
Ni wito wetu kwa timu nyingine za Ligi Kuu, kama JKT Ruvu ya Pwani, Coastal Union ya Tanga, JKT Orjoro ya Arusha, Toto Africa ya Mwanza, Ruvu Shooting ya Pwani, African Lyon ya Dar es Salaam, Kagera Sugar ya Kagera, Prisons ya Mbeya, JKT Mgambo ya Tanga na Polisi Morogoro kujiandaa vizuri.
Maandalizi tunayozungumzia hapa ni pamoja na kucheza mechi mbalimbali za kirafiki na timu zenye uwezo mkubwa kisoka katika kipindi hiki kabla ya kuanza kwa ligi hiyo ili kuwapa uzoefu na hali ya kujiamini wachezaji.
Tunasisitiza hili kwa kuzingatia kuwa, ni siku 11 tu zimesalia kabla ya kuanza kwa ligi hiyo, hivyo ni wajibu wa viongozi na makocha wa timu hizo za Ligi Kuu kuziandaa vizuri timu zao ili kuwa shindani kwenye ligi hiyo badala ya ligi hiyo kuwa kama mali ya Simba na Yanga.
Tunamaliza maoni yetu tukizikumbusha timu umuhimu wa kutumia vizuri muda huu uliosalia kabla ya kuanza kwa ligi hiyo, tukiamini kama kila moja itakuwa bora, ndio ufanisi wa ligi yenyewe kiushindani.