HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
ijumaa, 14 septemba 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti
Mbaraka Mwinshehe alimuogopa Shem Karenga

Ambrose Jimmy

 

KWENYE utani wa jadi wa nchi hii katika kandanda kulikuwa na Yanga na Simba, zote za Dar es Salaam; na utani huu bado unaendelea hadi sasa. Kwenye muziki wa dansi kulikuwa na bendi za Morogoro Jazz na Cuban Marimba zote za mkoani Morogoro, Mji Kasoro Bahari.

Kwa nini utani huu wa muziki usiwe Dar kama ilivyokuwa kwenye kabumbu? Hayo ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu kwani hata kandanda ilianzia Uingereza na kuja kutukuka Brazil.

Utani huu wa mindule haupo sasa kwa kuwa bendi hizi ziliishakata kamba longi. Kama ambavyo Simba na Yanga zilivyo na wapenzi kila kona ya Tanzania ndivyo ambavyo bendi hizo nazo zilivyokuwa.

Bendi hizi zikijaza wapenzi lukuki kuanzia Morogoro kwenyewe, Dar es Salaam hadi Ruvuma; na mikoa mingine utanisaidia kuitaja mpenzi msomaji.

Hii ilitokana na umahiri wa Salum Abdallah (na Juma Kilaza baadaye) kwa upande wa Cuban Marimba na Mbaraka Mwinshehe Mwaruka kwa upande wa Morogoro Jazz (baadaye Super Volcano baada ya Mbaraka kuanzisha bendi yake); umahiri uliosababisha muziki wa bendi hizo kung’ara kwa kuzisikiliza na kuzicheza.

Baada ya Salum Abdallah kuaga dunia mwaka 1966 bado Cuban Marimba iliendelea kutamba, kukata mbuga na kung’ara chini ya Juma Kilaza (ambaye wanadai alikuwa shemeji yake Salum Abdallah ingawa utafiti wa suala hili sijaukamilisha) kwa tungo mbalimbali ikiwa ni pamoja na wimbo wa “Mary.”

Bendi hizi zilikuwa zikitungiana nyimbo nyingi za mafumbo na kukejeliana na wapenzi wengi na hasa wa mikoani wakijua ulikuwa uadui wa kweli lakini kwa utafiti nilioufanya kwa watu wa wakati huo wa nyuma wanasema ile ilikuwa geresha tu bali ilikuwa ni katika kuleta ushindani tu wa kimuziki lakini Kilaza na Mbaraka walikuwa maswahiba (wale wenye habari tofauti katika hoja hii wanaweza kuleta mchango wao ili tuufahamu ukweli).

Mbaraka alikuwa akienda mikoani kama rais wa nchi akiheshimika sana. Labda ukiwaondoa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Oscar Kambona, hakuna mtu alikuwa maarufu nchi hii kama Mbaraka miaka ya mwishoni mwa 1960 hadi miaka ya 1970.

Nadhani hadi sasa hajapatikana mwanamuziki aliyekuwa amekamilika kama huyu. Alikuwa akitunga nyimbo nzuri zenye mafundisho ya aina mbalimbali, kuanzia mapenzi, siasa na jamii; alikuwa akipinga gitaa la besi, rhythm na solo kwa utaalamu wa hali ya juu; alikuwa mtaalamu mno wa kupanga muziki kwa ujumla wake.

Lakini katika gitaa la solo kwa kipindi hicho cha nyuma hakuna aliyekuwa anaweza kujitutumua na kuweka ligi na yeye.

Wapenzi wake wakimuita Soloist Nationale; yaani mpiga solo bora nchini. Jina hili lilitamalaki kama lilikuwa la kwake na akiitwa hivyo hata alipokuwa katikati ya wanamuziki wenzake wa bendi nyingine na wanamuziki wote wakikubali kuwa yeye ndiye alikuwa nembo ya muziki wa Tanzania.

Itaendelea.



juu