KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), iliyokutana jijini Dar es Salaam juzi, imepitisha marekebisho ya kanuni kwa ajili ya ligi za mkoa na wilaya.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema, marekebisho hayo yametokana na mabadiliko ya mfumo wa mashindano uliofuta Ligi ya Taifa na kuwa hivi sasa kutakuwa na Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi ya Mkoa na Ligi ya Wilaya.
Alisema kutokana na marekebisho hayo ya kanuni, Ligi ya Wilaya itaendeshwa na vyama vya soka vya wilaya (DFAs), na Ligi ya Mkoa itaendeshwa na vyama vya soka vya mikoa (RFAs).
Alisema, mechi za mchujo (play offs), kutafuta timu zitakazopanda kwenda Ligi ya Mkoa, zitaendeshwa na RFAs wakati za kupanda Ligi Daraja la Kwanza zitakazohusisha mabingwa wa mikoa, zitasimamiwa na TFF.
Aliongeza kuwa ligi za madaraja yote zitachezwa mwaka mzima kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.