MIEZI mitatu baada ya Rais Jakaya Kikwete, kuingia madarakani, alikutana na wanachama na wafadhili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) jijini Dar es Salaam kuwashukuru; akahitimisha hotuba yake kwa kutoa rai muhimu kwa chama chake. Alipendekeza mambo mawili.
Kwanza, alishauri wanaCCM waache tambo za ushindi wa kishindo; waanze kufikiria namna ya kujipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Machi 2006, rais aliyekuwa amekaa madarakani kwa miezi mitatu tu alikuwa ameshaanza kuota ngwe ya pili - miaka mitano mbele; kabla hajatimiza ahadi hata moja miongoni mwa mamia ya ahadi alizotoa kwa umma wakati wa kampeni.
Pili, alipendekeza chama chake kiangalie namna ya kupata vyanzo halali vya fedha za uchaguzi. Maana yake, rais alikuwa anakiri hadharani kwa kinywa chake, kwamba CCM imekuwa inatumia fedha chafu katika uchaguzi.
Kukiri huko kulikuwa kunakwenda mbali kwamba sehemu ya pesa zilizotumika kufanya kampeni yake zilitokana na vyanzo vichafu. Lakini zaidi ya hayo, alikuwa anakiri na kutangaza hadharani kwamba hakuwa mjinga, bali alijua fika suala hilo la pesa chafu (za kifisadi) za uchaguzi katika CCM.
Ikumbukwe kuwa wakati huo alikuwa hajawa mwenyekiti wa CCM. Hivyo, tafsiri ya kauli zake hizo inaweza kuwa kama alikuwa analalamikia uongozi uliokuwapo, kwa kuendekeza pesa chafu kwenye kampeni za kichama na kitaifa.
Ilikuwa indiketa ya wazi kwamba zamu yake ikifika kuwa mwenyekiti wa chama, wanaCCM na Watanzania watarajie mabadiliko makubwa ya kimsingi. Alitaka kuonyesha kwamba angeweza kujitenga na uchafu wa zamani katika CCM.
Na kwa kuwa alishasema wakati akifungua Bunge kwamba tabasamu lake lisiwahadae watu wakadhani yeye ni kiongozi anayechekacheka tu, asiye makini, kauli hii iliongeza mimwenyo miongoni mwa rafiki zake, wapambe wake na wote waliopenda kujitambulisha kuwa wana ‘urafiki na rais.’
Tusisahau, kauli hii ilitolewa katika kipindi ambacho kiligubikwa na matukio makubwa ya ujambazi wa kutumia silaha jijini Dar es Salaam na sehemu nyingine nchini.
Ni kipindi ambacho baadhi ya wananchi walishaanza kulalamika kwamba serikali ndiyo inalea majambazi kwa kuwa baadhi yao ni wafadhili wa CCM; na kwamba baadhi yao waliombwa na wengine wakashurutishwa kuchangia kampeni za CCM.
Zilikuwapo tetesi pia kwamba baadhi ya watu wanaofahamika kwa ujambazi wa kutisha walishirikishwa moja kwa moja katika mikakati ya kupata pesa za kampeni za CCM, wakawa wajumbe wa vikao vya mikoa yao vya kuhamasisha wapiga kura na hata wakawa wajumbe wa kamati za mapokezi ya mgombea urais alipowasili kwenye maeneo yao, wakisuguana mabega na viongozi wa serikali.
Hawa walikuwa majambazi wenye baraka za serikali, na mazingira haya yaliipa serikali ya awamu ya tatu sura ya kijambazi. Na yalimpatia Rais wa Awamu ya Nne fursa ya kusahihisha makosa, kujenga CCM mpya, kujitenga na uchafu wa watangulizi wake, na kutumia vema imani ya umma wa Watanzania kujenga Tanzania mpya.
Na kwa kuwa alikuwa na chagizo la kauli mbiu ya ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya (ANGUKA), kila mtu alijua kuwa Kikwete angewainua walioanguka na kujenga yaliyobomoka. Bahati mbaya ni kwamba anguka imemwangusha yeye!
Wafuatiliaji wa makala zangu watakumbuka kwamba niliwahi kumnukuu Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akisema nyumbani kwake Mwitongo, Butiama, mwaka 1995, wakati wa uchaguzi wa ndani wa CCM uliowapitisha Benjamin Mkapa, Cleopa Msuya na Jakaya Kikwete, kwamba kitendo cha kuwaengua wagombea wengine na kubakiza watatu hao ulikuwa ushindi mnono dhidi ya ‘pesa za bangi.’
Mwalimu Nyerere alisema kwa uchungu kwamba ‘baadhi ya wanaCCM walikuwa wanataka kutuwekea mgombea urais kwa kutumia pesa za bangi, lakini tumezishinda.’
Ukichanganya kauli ya pesa za bangi ya Mwalimu Nyerere na hii ya vyanzo vichafu vya pesa za uchaguzi ya Rais Kikwete, ni dhahiri utaona kuwa tabia ya viongozi kununua madaraka kwa pesa chafu ilianza mapema; walau ilichomoza miaka takriban 10 kabla ya Kikwete kuteuliwa na kuchaguliwa.
Hata Rais Kikwete alipoanza kuzungumzia na kuonya kuhusu hatari inayolinyemelea taifa, ya watu wenye pesa kutaka ‘kununua urais’ wa Tanzania, alikuwa akizungumzia mazingira hayo.
Lakini yalikuwa yakimsuta yeye mwenyewe kwa sababu taifa zima lilishuhudia ununuzi na ulanguzi wa kura uliofanyika kwa ‘takrima’ iliyokithiri na matangazo makubwa ya CCM ya gharama kubwa mno mithili ya bidhaa mpya sokoni.
Baadhi ya wananchi tuliojua kidogo kuhusu uchafu wa pesa za kampeni yake, tulimuona na yeye kama mlanguzi wa urais, si kwa pesa yake wala kwa mikono yake, bali kwa pesa ya wenzake – safi na chafu.
Na kwa kutambua ukaribu wake na baadhi ya wachangiaji wakuu wa kampeni zake, baadhi yetu tulitilia shaka uzito wa kauli yake.
Lakini wapo waliodhani kwamba angeweza kufanya kile kilichofanywa na Rais wa Malawi Bingu wa Mutharika, ambaye aliingia madarakani kwa wizi wa kura; na alipofika madarakani akawageuka walioiba kura ili ashinde, akasema, ‘sikuwatuma, sihusiki, na nitawashughulikia.’
Bingu alipoona mambo yamekuwa magumu, akaondoka kwenye chama tawala, akaanzisha kingine. Wahafidhina wakabaki kumshangaa, viongozi waandamizi na wastaafu wakamtenga kisiasa, wananchi wa Malawi wakamuunga mkono.
Kwa wakati ule, hata Rais Kikwete angeweza kufanya lolote, umma ungemuunga mkono; maana alikuwa bado anapendwa na watu wengi. Wachache walimtilia shaka.
Jeuri ya kujifanya anachukizwa na vyanzo vichafu vya pesa za uchaguzi ilitokana na ukweli kwamba alikuwa anaona na kuhisi jinsi umma ulivyomuunga mkono.
Alijua kwamba hata bila michango michafu 2010, jina lake pekee lingetosha kumvusha kirahisi katika uchaguzi.
Leo hii tunaporejea matukio na kauli zote hizo, tunashangaa kwa nini Rais Kikwete, ambaye sasa ni mwenyekiti wa CCM, ameshindwa kuwanyang’anya majambazi chama na kukirejesha kwa wanachama wakulima na wafanyakazi, wanaowakilishwa na jembe na nyundo.
Mivutano na minyukano iliyomo ndani ya CCM sasa inaweza kupata tafsiri nyingi; lakini mojawapo ni kwamba kuna mapambano ya matabaka ndani ya CCM – wenye pesa na wenye itikadi.
Wenye pesa hawako salama bila kuwa na sauti katika chama na serikali, na wenye itikadi hawako tayari kuzidiwa kete tena kwa sababu ya umaskini wao na kutumika kama mihuri ya kupitisha na kutetea masilahi ya matajiri wa CCM.
Na kwa kuwa wameshajua vidonda vya utawala mpya, wanavitonesha kuidhuru na kuilegeza nguvu, kwa madai kwamba wanapambana na ufisadi – hasa kwa kuwa wanajua kuwa baadhi ya mafisadi ndio hao wanaoipa serikali kiburi, na ndio wana sauti katika chama.
Baadhi ya wapambanaji hawa wa ufisadi ndani na nje ya CCM wanajua fika nguvu ya mafisadi katika uendeshaji wa serikali. Wengine wana orodha ya wateule wa serikali waliopata nyadhifa kubwa walizonazo kupitia uwakala wa mafisadi.
Ushawishi wa mafisadi kwa viongozi wakuu serikalini ni kitisho kingine ambacho wapambanaji wa ufisadi wanaamini kwamba ni mnyororo wa ziada unaokamata mkono wa rais katika kuwashughulikia.
Anawaamini rafiki zake wasioaminika kwa umma, huku pia akijaribu kuwasikiliza wanachama wa kawaida na wananchi wanaopiga kelele za ufisadi, huku nao wakitafuta huruma ya vikao vikuu vya chama, na kudai wanamsaidia rais kupambana na ufisadi.
Matokeo yake rais anakatika msamba wa kisiasa. Anaogopa kuwafagia mafisadi, lakini pia anaogopa kuwakemea wanaowasumbua mafisadi wake. Anakuwa popo; si mwenzao, si mwenzetu!
Lakini kwa kushindwa kuonyesha yuko upande gani, kwa kushindwa kutoa msimamo wa kiuongozi, rais anakuwa amewalinda mafisadi kwa sababu wana mabavu ya pesa na wana ushawishi katika mfumo wa utawala.
Bila kujua, anajikuta na yeye ameendeshwa na matakwa yao. Anajikuta mfukoni mwao, yeye na serikali yetu.
Tatizo kubwa na sababu ya kushindwa kwake vinatoka kule kule tulikoanzia – kwenye uchaguzi wa 2005; kwamba rais hawezi kuukata mkono uliomlisha.
Baadhi ya watetezi wake wamejaribu, na wanaendelea kuthubutu kusema bila mafanikio, kuwa pamoja na ukweli kwamba baadhi ya mafisadi wakubwa wamekuwa karibu naye kwa muda mrefu, yeye binafsi hakujua mapema kwamba pesa walizomchangia zilitokana na ufisadi.
Lakini kauli yake ya Machi 2006 inafuta utetezi wao huu. Tusisahau pia rais aliwahi kusema anawajua wala rushwa na kwamba anawapa muda wajirekebishe.
Aliwajua, na alitaka chama kiweke utaratibu wa kuwadhibiti. Rais Mkapa akafanya uamuzi mapema, akamwachia chama ili aone kama anaweza kutimiza azima yake.
Swali ambalo wananchi wanajiuliza leo ni kwanini mtu aliyejua hayo yote, na aliyetamka hayo hadharani, ameshindwa kujitenga na mafisadi na kuchukua hatua kali dhidi yao, na sasa wamemtafuna yeye na umaarufu wake wote?
Na kwa kutazama mikakati ya sasa ya CCM kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwaka kesho, ni nani anayeweza kudanganyika kwamba CCM haihitaji pesa zao chafu?
Kauli na mienendo ya mawaziri, ambao baadhi yao hawawezi kushinda bila kuhonga, lakini hawana vyanzo vya kuaminika vya pesa za kampeni, vinatupa ujumbe gani sisi tunaotarajia serikali iwashughulikie mafisadi?
Je, ile haraka ya Rais Mkapa kumwachia chama Rais Kikwete ilikuwa mtego wa kisiasa ili kulinganisha kauli zake na matendo yake?
Rais Kikwete aliyetoa hotuba nzuri iliyojaa vijembe kwa watangulizi wake siku alipofungua Bunge Desemba 30, 2005, Dodoma, pamoja na hii ya kulaumu vyanzo vichafu katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, ameshindwaje kutekeleza mambo hayo akiwa na madaraka yote mikononi mwake?
Je, anashindwa kuwashughulikia mafisadi kwa kuwa pesa halali hazitatosha katika uchaguzi wa mwaka kesho, na kwa kuwa jina lake pekee halitoshi tena kumvusha kama alivyodhani mwaka 2006?
Je, sasa ameanza kuona ‘hekima’ ya watangulizi wake kuendekeza pesa chafu katika uchaguzi? Inawezekanaje akaongoza serikali inayopigana kufa na kupona, na hata kuruhusu wateule wake kutumia rasilimali za taifa kuwatetea mafisadi kwa nguvu zote?
Wanaofuatilia mwenendo wa kisiasa nchini, wakatazama hamasa ya wananchi katika maeneo mbalimbali, wanaona umma ukiwa nyuma ya rais na chama chake katika vita dhidi ya ufisadi?
Wanajiuliza, kwa nini wananchi wamemkimbia aliyekuwa mtu wao? Je, sasa tukubali ile nguvu ya pesa za bangi alizosema Mwalimu Nyerere ndiyo imewashinda watawala?
Je, watawala walioshindwa na nguvu ya pesa ya bangi wanaweza kuiokoa serikali yetu isiingizwe katika mifuko ya mafisadi? Tukisema mafisadi wameiweka serikali mfukoni, serikali itakuwa na haki kutulalamikia?
Tunajua imeshindwa kujinasua. Je, iko tayari tuisaidie na kuiondoa mifukoni mwa mafisadi? Au itatuhukumu na kutugeuzia kibao kwa kutumia sheria mbovu dhalimu, za kikoloni? Tutaendelea kuulizana.