HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumapili, 31 mei 2009
Yaliyopita
Pekua Tovuti
Wasiliana na Mwandishi
+447984584292
ansbertn@yahoo.comTuma barua-pepe
www.ngurumo.blogspot.comTembelea blogu
Fisadi mmoja, mawaziri 10

Ansbert Ngurumo

 

LEO nina hoja mbili zinazojitegemea, lakini nitazijadili katika makala moja kwa kuwa zimejitokeza katika wiki moja, na zinaweza kutufundisha namna ya kuiambia serikali, ‘hapana!’

Nilipoandika wakati fulani kuwasifia wananchi wa Tarime kwa nguvu ya kimkakati, kiakili na kimwili waliyotumia kushinda nguvu na hila za dola katika uchaguzi mdogo uliopita jimboni mwao, kuna watu ambao hawakunielewa.

Naamini sasa wamenielewa, baada ya matokeo ya uchaguzi mdogo wa Busanda mkoani Mwanza. ‘Hapana’ iliyosemwa Busanda haikuwa na kishindo kizito kama cha Tarime.

Wananchi wa Busanda walizomea lakini hawakuchukua hatua ya ziada. Hawakutunisha misuli, na matokeo yake, wao ndio waliopigwa na washindani wao – mbele ya vyombo vya dola.

Mamia ya askari waliomwagwa Busanda hawakuwa na kazi kubwa kwa sababu hawakukabiliana na upinzani mkali wa kimabavu.

Hata hivyo, askari hao walitimiza matakwa ya kimkakati ya CCM ya kuwa tishio linaloonekana kwa wapiga kura.

Kwa sababu ya unyonge na upole wa wana Busanda ambao silaha pekee ilikuwa ni kuzomea, CCM ilitumia wahuni wake kuwapiga wazomeaji, wananchi washindani wa chama tawala.

Tofauti na Tarime, wajumbe wa CCM waliokamatwa katika uandikishaji au ununuzi wa shahada za kupigia kura kinyume cha sheria hawakupewa mkong’oto; wala polisi au Tume ya Taifa ya Uchaguzi hawakuchukua hatua kali kuwaadhibu wahusika au waliowatuma.

Wala Tume ya Uchaguzi haikujali malalamiko dhidi ya wanaogawa ‘takrima’ wakati wa kampeni au vitisho vya Waziri wa Nishati na Madini (William Ngeleja) kwa wapiga kura; na matukio mengine ya aina hiyo yaliyovunja sheria za uchaguzi moja kwa moja.

Hata leo, naamini tume haijatoa maelezo kuhusu upungufu wa wapiga kura kutoka 135,000 waliojiandikisha hadi 52,000 waliopiga kura. Haitaki kuuliza au kujiuliza kwa sababu bila shaka inajua idadi hiyo ilikopotelea.

Ni wazi kwamba waliogombea wakiwa wapinzani wa CCM walikuwa wanapambana na serikali iliyowakilishwa na vyombo vya dola. Kwa hiyo, katika mazingira hayo, kilichotokea ndicho tulichotarajia.

Hata washindi wanajua kuwa kama ingetumika nguvu ya umma kama ya Tarime, wasingeshinda Busanda hata kwa kura hizo chache zilizopigwa! Kwa sababu hiyo, naamini washindani wa CCM wamejifunza somo la ziada huko Biharamulo wanakokwenda.

Kama wataweza kudhibiti nguvu ya mtandao wa CCM inayopunguza idadi ya wapiga kura; kama wataweza kudhibiti na kukabili vitisho vya polisi na wahuni wa CCM; kama wataweza kuwachukulia hatua pale pale wanaojihusisha na kugawa ‘takrima’ wakati wa kampeni, wanaweza kuongeza fursa ya ushindi.

Lakini kwa hali hii, kuna hoja ya ziada. Tangu uchaguzi wa Tarime, tumeanza kuamini kuwa umoja wa wapinzani si njia pekee ya ushindi dhidi ya CCM. Tusiwalazimishe wapinzani kuungana. Tuwaache wajipime kukubalika kwao, kwani kila chama kina sera zake, na kina nia ya kutwaa madaraka.

Wakati mwingine, hata wakiungana hawawezi kushinda. Zaidi ya hayo, wanaoungana lazima waunganishe nia. Imeshadhihirika sasa kwamba wenzetu hawa hawana nia moja. Upo uwezekano kwamba wakiungana watahujumiana. Bora wabaki walivyo kuliko kuwa na ushirika wa mashaka.

Lakini wajue kuwa wanaposhindana na CCM wasitarajie kushinda majukwaani tu. Umuhimu wa majukwaa upo pale pale, na wameyamudu sana. Wameiondoa CCM majukwaani. Lakini kule ilikokimbilia kujificha ndiko ziliko kura wanazohitaji kushinda.

Kwa sasa, tutawapongeza CCM kwa ushindi, hata kama ni wa goli la mkono, na tuwahoji kama wabunge wanaotupatia wanaongeza nguvu yoyote bungeni au wanaongeza tu idadi ya kufanyia mbwembwe.

CHADEMA nao wanastahili pongezi. Mwaka 2005, katika jimbo hilo hilo walipata kura 3,000 tu.

Kama wameweza kuzoa kura zaidi ya 22,000 katika mazingira magumu kama haya, ina maana chama kinazidi kukua na kukubalika kwa wananchi.

Na wajue kuwa huko tunakoelekea, kama wanataka kusema ‘hapana’ waseme hapana ya kweli, yenye kishindo kama cha Tarime. Vinginevyo, wataendelea kusindikiza.

Hoja yangu ya pili leo inanirejesha miaka 18 iliyopita, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliposema serikali dhaifu hukwepa kukusanya kodi kutoka kwa matajiri, na huishia kutanua misuli yake kwa kufukuzana na watu wadogo wadogo.

Mwalimu alikuwa sahihi. Na alisisitiza kuwa serikali ya namna hiyo ndiyo huendeshwa na matajiri, ambao hudai na hudiriki kuiweka mfukoni.

Na wanapoiweka serikali mfukoni, maana yake ni kwamba wananchi nao wamo mfukoni pia.

Maana pana zaidi ni kwamba mifuko ya wananchi inakuwa na matobo makubwa makubwa ambayo yanatobokea kwenye mfuko huo wa matajiri.

Maskini watazidi kuwa maskini, na matajiri watazidi kuwa matajiri. Lakini kinachogomba si utajiri wao, bali jinsi wanavyoupata kwa jasho na damu ya wananchi maskini walipa kodi, ambavyo haviwarudii katika mfumo wa huduma za msingi wanazostahili.

Watafiti na wataalamu wa masuala ya kiuchumi na kijamii watatueleza kama miaka 18 iliyopita imeshuhudia maskini wakiinuka au wakididimia zaidi. Watatueleza kama matajiri wachafu wameongezeka au wamepungua. Watatueleza kama serikali yetu imewatumikia wananchi au matajiri.

Watatueleza kama nchi hii inaongozwa na watawala tuliowachagua au matajiri waliojificha nyuma ya mgongo wa wanasiasa; watu wenye pesa safi na chafu walizopata kwa ujanja na wakazitumia kwa ujanja kutuwekea watawala watakaolinda masilahi yao.

Lakini hata kabla ya utafiti huo kufanyika, wananchi wameshagundua matabaka ya matajiri na maskini yaliyoibuka kwa kasi ya kutisha katika miaka miwili iliyopita ya vita ya ufisadi ilipopamba moto.

Na baadhi ya watafiti wanaweza kuthibitisha hata sasa kuwa uchumi wa nchi hii haumilikiwi na serikali, wala hauko mikononi mwa wananchi wa Tanzania.

Haipendezi, na wengine hawataki isemwe, lakini ukweli ni kwamba uchumi wa nchi hii uko mikononi mwa wageni na kikundi kidogo cha Watanzania wenye asili ya kigeni, na wazawa wachache sana ambao, kwa sehemu kubwa, kufanikiwa kwao kumetokana na ukaribu wao na vikundi hivi viwili.

Kwa kuliona hili na kujaribu kulizuia, wanaharakati na wanasiasa waasisi wa Chama cha NCCR-Mageuzi, walibuni sera ya uzawa, ili kuilamzimisha serikali iwape wananchi wazawa upendeleo maalumu na uwezeshaji wa makusudi katika kumiliki uchumi wa nchi yao, na kuwaondoa katika hisia za ukoloni na utumwa.

Kwa kuwa hawakushinda kushika madaraka ya dola mwaka 1995, NCCR-Mageuzi hawakuweza kutekeleza sera hii; na migogoro ya kisiasa iliyowakumba baada ya hapo, ndiyo iliyotafuna mvuto wa sera yao, ambayo iliibuliwa kwa staili nyingine na aliyekuwa Mbunge wa Ilala, Iddi Simba.

Lakini naye hakudumu nayo, kwani chama chake kilimshambulia kutoka pembe zote; na hata pale walipohisi anautaka urais, wakamuwahi na kumshughulikia kiufundi kupitia sakata la vibali vya sukari.

Ingawa Simba alitekeleza suala hilo akiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, kwa makubaliano na Rais Benjamin Mkapa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge; ni yeye aliyebeba msalaba peke yake. Akatokomea na sera yake ya uzawa.

Nguvu ya matajiri wenzake wazawa na wasio wazawa ilipenyezwa kwenye ulingo wa siasa, ikammaliza kisiasa.

Ama alijua au hakujua kwamba baadhi ya washindani wake hawakuwa na nguvu ya kifedha kwa ajili ya kampeni, bali waliweka matumaini yao katika mifuko ya ‘wenye nazo’ – na kwa kiasi kikubwa waliweza kufanikisha yote waliyopanga.

Sasa hao ‘wenye nazo’ ndio wamechomoza katika orodha za wale wanaotajwa tajwa katika kashfa za kifisadi.

Baadhi yao ndio hao waliotuhumiwa kuwa mafisadi papa, serikali haikuona aibu kujitokeza kuwatetea kwa kutumia vyombo vya umma na rasilimali za umma.

Ilikwenda mbali hata kudiriki kuwatisha wananchi kwa kutumia vyombo vya dola, kuwaziba midomo kwa kisingizio cha kufunga mjadala ambao haikuuanzisha; na kupandikiza hisia za kijinga kwamba anayewatuhumu wengine ni mbaguzi wa rangi.

Lakini tafsiri ya hatua hizi za serikali iko wazi kabisa. Na wananchi sasa wanajua nani anaiendesha serikali, nani ameishika mikono na midomo. Ni yule aliyeshika uchumi wa nchi.

Nakubaliana na uchambuzi wa mtu mmoja aliyesema kwamba nyuma ya kila fisadi papa mmoja, kuna mnyororo wa watu kama 500 waliofaidika, wanaofaidika, au wanaotarajia kufaidika na rasilimali zake kijamii au kisiasa, na baadhi yao wanaongozwa na mawaziri.

Na hawa ndio wanafanya jitihada za kufa na kupona kudhoofisha na hata kuua harakati za vita dhidi ya ufisadi – maana baadhi yao wamo serikalini.

Umaskini wao wa kimawazo na kifedha umekuwa mzigo mzito mioyoni mwao, na umepofusha hata akili zao, kiasi kwamba wapo tayari kuidhalilisha serikali kwa kutunga sera zenye ‘harufu’ ya utetezi au mashambulizi ya mtu mmoja!

Kama fisadi mmoja ana uwezo wa ‘kumiliki’ mawaziri zaidi ya 10, akawawekwa sawa watendaji wa vyombo kadhaa vya dola, akawateka wanahabari kadhaa; akawaajiri wapambe na wapiga debe wa kumsafisha au kumchafulia wagomvi wake; akawashawishi watu muhimu wamfungulie milango ya ofisi nyeti za serikali; tunatarajia mafisadi 10 watamiliki sehemu gani ya utajiri wa taifa?

Katika miaka miwili iliyopita tuliona jitihada za serikali na wapambe wake kufinyanga finyanga kile walichokiita muswada wa uhuru wa habari katika jitihada za kuwabana wawekezaji, wamiliki na watendaji wa vyombo vya habari kwa kuwapatia kamba ndefu ili wajinyonge wenyewe!

Wadau wakaukataa muswada kwa kutoa sababu za kitaalamu. Leo hii, serikali imekuja kwa mbinu nyingine ya kutunga sera ya habari na mawasiliano ambayo ndani yake mna vipengele vinavyoonekana kuwalenga watu binafsi wasiozidi wawili katika nchi ya watu milioni 40!

Kwa mfano, pendekezo la serikali kwamba mtu mmoja asimiliki vyombo kama televisheni, redio au magazeti kwa wakati mmoja eti kwa kuwa anaweza kutumia vibaya na kuathiri jamii, ni hoja ya kipuuzi, ya kitoto na ya kifisadi.

Ni ya kinafiki zaidi kwa serikali ambayo inatumia vibaya vyombo vyetu vya umma kwa ajili ya kufanyia kazi za serikali na wakati mwingine kutetea watuhumiwa wa ufisadi, huku ikijipa jukumu la kuhukumu wengine kwamba wanatumia vibaya vyombo vyao.

Serikali inayoshindana na wananchi wake hata katika kufanya biashara, haiwezi kuwahukumu washindani hao hao ikaaminika.

Inaeleweka wazi kuwa vyombo vya binafsi vimesaidia kupiga vita ufisadi unaowaneemesha baadhi ya watendaji serikalini.

Kwa hiyo, inapowashambulia wenye vyombo binafsi vya habari hata kuwatungia sera, inaonyesha udhaifu mkubwa na uwezo mdogo sana wa kufikiri wa watendaji wa serikali.

Zaidi ya hayo, inaonyesha wazi nia mbaya ya watawala, kwamba hawajali masilahi ya umma; na inadhihirisha utoto wa waandaaji wa sera hiyo kwa kudhani kwamba wao wataishi na kufia serikalini.

Hii ndiyo tabia ya serikali iliyowekwa mfukoni mwa mafisadi niliyoijadili wiki iliyopita. Na haya ndiyo madhara yake kwa umma wa wananchi maskini, wanyonge na wanyenyekevu.

Bahati nzuri inayojitokeza ni kwamba miongoni mwetu wapo watu, mmoja mmoja au makundi, wanaoweza kuiambia serikali: ‘hapana!’ Hii ni hapana ya kweli. Ole wake serikali kama haiwezi kuelewa maana ya kauli hii ya wadau.



juu