UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umepokea msaada wa kompyuta 30, printa na projekta moja vikiwa na thamani ya zaidi ya sh milioni 30.
Akikabidhi msaada huo jana, Balozi wa Sudan nchini Tanzania, Abdelbagi Kabeir alisema, msaada huo unatokana na ahadi aliyoitoa mwanzoni mwa mwaka huu kwa vijana hao walipokutana na uongozi wa vijana wa nchi ya Sudan, baada ya kufikia makubaliano ya kuanzisha vituo viwili zaidi vya kompyuta.
Alisema lengo ni kuendeleza ushirikiano na mshikamano wa nchi hizo mbili katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
“Lengo ni kuendeleza mshikamano uliopo baina ya nchi hizi mbili na tutawaunga mkono kwenye vituo vingine zaidi,” alisema Kabeir.
Naye Katibu Uhamasishaji na Chipukizi wa UVCCM Taifa, Esther Bulaya, alisema CCM ina mahusiano mazuri na vyama vingi Afrika, ikiwamo chama kinachotawala nchini humo.
Alisema vituo hivyo viwili vitatumika kwa kufundishia makada wa CCM na wale wote watakaohitaji huduma hiyo kwa ada nafuu.
“Vituo hivyo vitatumika kwa kufundisha makada wa CCM na wale wote watakaohitaji huduma hii kwa ada nafuu, ambapo pia itasaidia katika kuimarisha mtandao wa UVCCM nchi nzima kwani mawasiliano yatakuwa kwa kompyuta, yaani mtandao,” alisema Bulaya.