NIMEFARIJIKA kwamba kishindo cha mapambano yetu dhidi ya mafisadi wiki hii kimetokea katika kinywa cha Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi akisema: “Walijipenyeza kupata madaraka, sasa wameshikwa pabaya, wanaumbuka!”
Kuna anayetilia shaka kauli ya Mzee Mwinyi aliyoitoa juzi, katika Jimbo la Same Mashariki? Tafakuri ya haraka haraka, inaonyesha kwamba kauli hiyo ina maana mbili.
Kwanza, Mzee Mwinyi anaungana na wananchi katika kusisitiza kwamba mafisadi si wananchi wa kawaida tu, bali ni viongozi wenyewe ambao yeye amewaita ‘waliojipenyeza kupata madaraka.’
Inaua kabisa propaganda za watawala na jitihada zao za kujivua ufisadi majukwaani na kwenye vyombo vya habari. Inasisitiza kile ambacho watawala wamekuwa wakihaha kukipinga kwa miaka miwili mfululizo, hadi wakazomewa na hata ‘kupigwa mawe’ mikoani.
Mzee Mwinyi yumo katika kundi la watawala, lakini anajipambanua na wenzake kwa mwenendo wake wa maisha na kwa kauli za kiutu uzima na kiungwana kama hizi. Ni kauli inayotolewa kwa upole wa hulka ya msemaji mwenyewe, lakini yenye makali yanayokata kuwili kama wembe.
Baadhi yetu tunajua kuwa kutokana na usafi, uungwana na upole wa Mzee Mwinyi, mafisadi hawahawa wamediriki kumweka karibu na kumshirikisha harakati zao ili awaunge mkono katika kuingia na kudumu madarakani.
Na baadhi yao wamefaulu kumfanya sapota wao wakati fulani, lakini naye ni mtu mzima; anaona na kusikia yanayomzunguka. Anajua kuwa kubebana ni jambo la kawaida katika maisha, hasa katika siasa wanazofanya wao; lakini wanasiasa wengine hawabebeki. Je, ameamua kuwabwaga chini vijana wake?
Mzee Mwinyi halazimiki kuendelea kuwabeba wanasiasa wanaochana mbeleko. Na kwa kauli yake ya juzi, ametoa ashirio jipya kwamba watawala ambao wamekuwa wanamtegemea sasa wamekomaa, wajitegemee, wajitetee na wawajibike kwa maamuzi na matendo yao.
Amesoma alama za nyakati. Anajua kuwa pamoja na kwamba wanavaa suti za gharama na kunawiri, wanakula na kusaza na hata kukufuru kwa ‘kuvimbiwa’, wanatumia na kutumbua kodi za wananchi kwa mbwembwe, wanatabasamu na kucheka kwa kejeli; upepo wa kisiasa unavuma dhidi yao.
Baadhi yao wamefikia mahali ambapo fursa pekee ya furaha moyoni wanayoipata ni pale wanaposafiri nje ya nchi, mahali wasipotazamana na wananchi wenye njaa, maradhi, umaskini, hasira na maswali magumu.
Mzee Mwinyi anayasema haya kwa walio madarakani na wastaafu ambao wanaishi kwa aibu, woga na vitisho; ambao hawawezi kujinasua katika ufisadi bila ‘kujichuna ngozi’ ya kisiasa.
Ni vema kwamba mtawala mwenzao, tena mzoefu na mkongwe kuliko wao, anayasema haya hadharani.
Pili, kauli hii ni tangazo jingine kutoka kwa Mzee Mwinyi kwamba amehama kambi. Ameamua kujitenga na kundi la wengi ndani ya CCM ambao wanawasemea wachache. Anajiunga na wachache wanaowasemea Watanzania walio wengi.
Katika kipindi ambacho mwenyekiti wake wa CCM amekiri kwamba mafisadi wameizidi ujanja serikali yake, huku katibu mkuu wa CCM akijipendekeza kwa watu wale wale aliowachachamalia siku chache zilizopita; kauli ya Mzee Mwinyi ni ishara ya ushindi wa kundi dogo lenye nguvu ndani ya CCM – kundi la wapambanaji akina Samuel Sitta, Dk. Harrison Mwakyembe, Lucas Selelii, Anne Kilango Malecela, Aloyce Kimaro na wengine ndani ya CCM ambao kauli zao zimewafanya waonekane kuwa maadui wa chama ndani ya chama, hadi kutishiwa uanachama na hata uhai wao.
Tatizo la kauli yake ni moja. Inawakera watawala na viongozi wa chama chake. Na haijakisaficha chama chake. Bado kitaendelea kuitwa ‘chama cha mafisadi;’ si kwa sababu viongozi wote au wanachama wote wa CCM ni mafisadi. La hasha!
Tunajua kwamba wapo viongozi wa CCM ambao si mafisadi. Lakini hawana nguvu. Na licha ya kwamba ni viongozi, si wao wanaoendesha chama.
Enzi za viongozi waadilifu kuendesha chama zilikuwapo wakati chama kikizingatia na kufuata kanuni, taratibu na imani ya chama na miiko ya uongozi. Nguvu yao ilikwisha pale mambo hayo yalipopinduliwa na kufunikwa na takrima, ambayo ndiyo imekuwa inazalisha makundi ya viongozi wanaoshikilia madaraka serikalini na katika chama kwa sasa.
Takrima hii ndiyo imezaa ufisadi wa kitaasisi ndani ya CCM kwa kuwa ndiyo imekifanya chama kuongozwa na mafisadi. Ama walichanga pesa nyingi au walichangiwa pesa nyingi safi na chafu wakati wa kampeni, na wanahaha kuzirudisha wakiwa madarakani.
Kwa sababu hiyo, chama kimekamatwa na mafisadi; hivyo si rahisi kuwachukulia hatua. Kwenye maandishi ya kuvutia wanachama wapya na kujiuza kwa wananchi, CCM kinasema: “ni rahisi kujiunga na CCM kwani masharti yetu yanamlenga mwananchi yeyote mwadilifu.”
Lakini wananchi wanaojua yanayoendelea ndani ya chama hicho, yakisimamiwa na viongozi wake, hawawezi kuishia katika kusoma tangazo hilo la masharti ya uanachama wa CCM.
Ndiyo, hayo yalikuwa masharti ya uanachama katika CCM ya Mwalimu Julius Nyerere. CCM ya Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete haifanani na masharti hayo; wala haiwezi kujigamba kwamba inazingatia kanuni ya mwiko wa rushwa na fitina za kisiasa.
Chama ambacho kinatumia mfumo wake kutetea na kulinda baadhi ya mafisadi na kutosa baadhi yao; chama ambacho kinaogopa baadhi ya mafisadi hadi kutumia vyombo vyetu vya usalama wa taifa kuwapatia ahueni ya kisiasa na kibiashara, hakiwezi kujivua jina baya kama hilo.
Ndiyo, kama anavyosema Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, ufisadi wa CCM ni wa baadhi tu ya wanachama si wa wote, lakini nguvu inayotumika kuwalinda ni ya chama na serikali. Maana yake ni kwamba wakubwa au chama chenyewe kina maslahi binafsi katika ufisadi wa wanachama hao ambao Makamba anawaita ‘mmoja mmoja.’
CCM inayopambana na ‘dagaa na sato’ wa ufisadi huku ikiwaogopa na kuwalinda ‘mapapa’ wanaofahamika na wenye nguvu ndani ya chama, haiwezi kamwe kujivua gamba la ufisadi, hata kama ndani ya chama hicho kuna wapambanaji makini na jasiri wasiotetereka.
Ama wanatetea maslahi yao; au wanataka kurejesha heshima ya chama; au wanataka kulinda maslahi ya taifa au vyote. Lakini kinachotufanya wananchi tuwatambue na kuwapambanua akina Kilango, Mwakyembe na wenzao ni kwa sababu hawafanani na chama chao.
Kwani CCM kina wabunge wangapi? Mbona ni hao tu wanaosikika? Kwani CCM kina wastaafu wangapi? Mbona ni kina Mwinyi na (Waziri Mkuu Mstaafu Rashid) Kawawa wanaosikika na kusikilizwa?
Ni kwa sababu ni wana CCM wanaojitofautisha na CCM ya sasa; wanajitambulisha na CCM iliyopita ya waadilifu. Je, wataishia kutoa kauli tu au watatusaidia kuondoa mafisadi wanaoishikilia CCM na serikali?