logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumapili, 27 Januari 2008
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
sp.l_icon sp.r_icon
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1


Eti Ballali kalishwa sumu?
Ansbert Ngurumo


SIKU zipatazo 10 baada ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Daudi Ballali, kusemekana amepelekwa nje ya nchi kwa ‘matibabu,’ mtu mmoja aliniambia: “Huyo ameondoka. Hawezi kurudi. Akirudi hatakuwa gavana tena. We utaona.”

Sasa baada ya yaliyotokea kwa gavana huyo kutenguliwa uteuzi wake, sina shaka kabisa na nilichoambiwa na mtu huyo. Nimeamini kauli yake, na sihitaji ushahidi wa nyongeza.

Hii ina maana kwamba ingawa serikali inajaribu kutuficha mambo kadhaa, kuna watu wanaoyajua, hata kama hawajaamua kuyasema hadharani.

Na kama kuna mambo serikali hii iliyoonyesha kiwango cha juu cha ‘usanii’ ni hili la Ballali. Ajabu ni kwamba, licha ya usanii huo wa viongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, kama kuna jambo linafahamika, hata kwa wale ambao serikali haitaki walijue, ni hili la Ballali.

Mwanzoni ilijaribu kulifukia bungeni kwa kauli za Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, waliokataa katakata kuundwa kwa Tume ya Bunge kuchunguza ubadhirifu wa BoT.

Baadaye waipoona mtoa tuhuma, Dk. Wilbroad Slaa, ameng’ang’ana na hoja yake, wakamtumia Spika Samuel Sitta, kumtisha Dk. Slaa kwamba ana vielelezo feki, na kwamba watamshitaki kwa kughushi!

Lakini wapi! Ukweli ulishinda na hatimaye Rais amemfukuza kazi gavana yule yule wabunge waliyetueleza kwamba alipoitwa bungeni alitoa maelezo makini yaliyowaridhisha!

Yanayotokea sasa yanatufanya tuwe na shaka na kamati ya wabunge iliyomuhoji Ballali na kuridhishwa kirahisi na maelezo yake. Au nao walipewa kitu kidogo?

Tukubali kwamba kama si ujasiri wa Dk. Slaa, hata hiki kidogo kilichofanywa na serikali kisingefanyika. Na kwa kuwa haikuonyesha utashi tangu awali, ndiyo maana wananchi wanatilia shaka hata hatua hizi zinazochukuliwa kisiasa kupoza mambo, kwa lengo la kulinda hadhi za watu binafsi na kutosa usalama wa raia wengi.

Sina shaka kwamba tabia hii ya serikali kujaribu kuficha ukweli wa mambo yanayowahusu wananchi wake, ndiyo inayochochea watu kulipua hata yale ambayo wangekaa nayo moyoni. Na sasa, itarajie yatalipuka mambo ambayo yataishtua zaidi.

Na kwa kuwa haitaki kusema ukweli, basi iwaache wananchi waseme wanalojua au wanalohisi kuhusu Ballali.

Kitu kilicho wazi ni kwamba serikali inajua kuwa inatuhumiwa katika ufisadi unaomhusu Ballali.

Wapo wanaomtuhumu Rais mstaafu Benjamin Mkapa. Kama kiongozi mkuu wa serikali na mwajiri wa Ballali, hakuna shaka kwamba alijua matatizo ya BoT, lakini alikaa kimya!

Wengine wanasema si kwamba alikaa kimya, bali alihusika kwa namna fulani; ndiyo maana Ballali alijiamini kupita kiasi.

Wanaomtuhumu Mkapa wanamtazama Rais Jakaya Kikwete usoni. Wanataka kuona kama atachukua hatua zozote zitakazomgusa moja kwa moja Rais Mkapa. Wanakumbuka kauli yake bungeni Desemba 30, 2005 aliposema kwamba ingawa ana sura ya tabasamu, yeye ni mtu makini katika masuala mazito.

Haya sasa! Limejitokeza suala nyeti na zito la Benki Kuu ya Tanzania. Hii ni benki ya Watanzania. Imevurugwa kwa wizi wa kutisha kutoka kwa vigogo. Wezi wanafahamika. Waliowatuma na kuwaagiza wanafahamika.

Rais naye ni sehemu ya vigogo. Lakini ndiye mwenye mamlaka ya kuchukua hatua. Kama Rais anataka tumuone makini, huu ndio wakati wake.

Tumesema na tutarudia. Kama amekuwa na ujasiri wa kumtosa Ballali, hawezi kukosa ujasiri wa kuwatosa wengine waliosaidiana na Ballali. Bahati nzuri, wengine ni watumishi wa umma hadi sasa. Hivyo, ana mamlaka ya kuwatimua kama Ballali.

Tayari wenye akili wameshamweleza Rais kuwa Ballali hawezi kufukuzwa peke yake likaonekana jambo la kishujaa, kwani hakufanya ‘uhuni’ huo peke yake. Kinachosemwa sasa ni kwamba serikali inajidai imemtimua Ballali wakati mwenyewe alishajiondoa na kukimbilia nje ya nchi.

Inasemekana alishajiuzulu. Kwa hiyo, Rais Kikwete amefukuza kivuli! Ballali hakuwapo tena! Sasa Rais aonyeshe makali yake, afukuze walio kazini, aache kukimbizana na vivuli.

Serikali hii imejikita katika uongo. Rais, mawaziri wake, watendaji wa BoT na hata watu wa Usalama wa Taifa wanasema hawajui hospitali aliko Ballali. Halafu wanataka tuwaone makini?

Kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alilazwa na tukaambiwa yuko Hospitali ya Mt. Thomas, London; iweje Ballali anayetuhumiwa alazwe katika hospitali ambayo hakuna mtu hata mmoja wa serikali anayeijua?

Tukiwaita waongo watachukia? Watasema tumewatukana? Tazama mwongo mwingine katika sakata hili: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, anayeshughulikia Utawala Bora, Philip Marmo, amesema wiki iliyopita: “Mimi nasikia tu kama wewe, sijui yuko wapi...”

Hawa ndio baadhi ya viongozi wasio na faida kwa taifa. Hivi mtu kama Marmo baada ya kusema uongo wa wazi kama huu, anatarajia siku nyingine atoe kauli jamii imwamini? Bahati mbaya, anasema uongo huu akiwa ofisini mwa Rais...

Na kwa sababu serikali inakataa kusema ukweli juu ya alikopelekwa Ballali, taarifa za uongo na kweli zinaanza kusambaa juu ya kilichomtokea Ballali.

Ikumbukwe kwamba Ballali mwenyewe alipokutana na waandishi wa habari mapema Septemba 2007, aliwaeleza kwamba afya yake ni nzuri kabisa! Ingawa yeye si daktari, ni nani angeweza kumsemea Ballali kuhusu afya yake mwenyewe?

Lakini siku chache baadaye, Ballali huyo huyo alisemekana kwamba ‘amepelekwa nje kwa matibabu!’ He! Kumbe afya yake haikuwa murua kama alivyosema! Au kuna kitu kilimtokea ghafla?

Wengine wakadai amepata shinikizo la damu kutokana na kishindo cha tuhuma za ufisadi. Baadhi ya maofisa wa BoT wakadai amekwenda kufanyiwa uchunguzi wa kawaida wa afya yake. Wapi? Wakasema hawajui!

Baada ya siku kuongezeka na mambo mengi kufunuka, zikaanza kuzuka tuhuma dhidi ya serikali kuhusu Ballali.

Ikaanza kusemekana kwamba serikali ndiyo iliyomdhuru Ballali. Wapo wanaosema kwamba baada ya kuona mambo yanaanza ‘kubumburuka’ na kwa kuwa wanajua ukweli wa mambo halisi, baadhi ya vigogo wanaohusika na tuhuma hizo waliwaagiza vijana wao ‘kumkolimba’ Ballali, ili kuua ushahidi!

Mh! Bahati nzuri hakufa, watu wake wakamkimbizia nje haraka kwa matibabu; na kwamba alifanyiwa operesheni kuondoa utumbo uliooza kwa sumu aliyolishwa! Na kwambia serikali inakaa kimya, na wananchi wanasema walijualo.

Mh! Eti kuanzia hapo, baadhi ya vigogo wamekuwa wakimtembelea hospitalini kutazama anaendeleaje, na serikali imekuwa inafanya kila mbinu asirejee nchini kutoa ushahidi; na kwamba hata hatua ya kumfukuza kazi, ni mkakati ule ule wa kumwondoa katika minyororo ya serikali na kumpatia uhuru wa ‘kupotelea atakako.’

Hakika, hakuna mtu mwenye akili atakayekubaliana na rais na wasaidizi wake kwamba serikali haijui aliko ‘mgonjwa wake.’ Kama ni kweli serikali haijui, basi hatuna serikali!

Bahati mbaya, serikali inafanya mambo haya kitoto. Inaposema ‘haijui’ hospitali alikolazwa, ni ushahidi mwingine kwamba inajua alipo. Inadhihirisha kwamba haiko makini.

Maana kama ingekuwa makini, na inataka sisi tuione makini, isingethubutu kusema haijui alipolazwa Ballali. Kila mtu anajua inaongopa. Kwa sababu hiyo, uvumi na tetesi vitaendelea.

Ni tetesi zinazoua sura nzuri ambayo serikali chafu inajaribu kujipatia katika sakata la Ballali na ufisadi. Ni tetesi zinazolenga kusisitiza kwamba wahusika si kina Mkapa tu, bali hata kina Kikwete na rafiki zao.

Maana inasemekana kiasi kikubwa cha fedha zilizochotwa kilikuwa na uhusiano na makampuni hewa ya watu walio ndani ya utawala wa sasa, kwa kuwatumia marafiki, jamaa na wajuani wao ili kuficha ushahidi.

Kigugumizi cha serikali na hatua yake ya kupapasa uchunguzi wa BoT bila kuhusisha ule wa pesa zilizopotelea kwa makampuni ya kitapeli ya Deep Green, Tangold, Meremeta na mengine yaliyohusishwa na CCM, ni ishara nyingine kwamba walio madarakani wanajua bomu la Ballali haliwezi kulipuka likawaacha wao wakiwa imara.

Kwa hiyo, wanachofanya sasa ni propaganda tu ili kunyamazisha kile ambacho Rais Kikwete amekiita “kelele za wananchi” juu ya suala la ufisadi.

Ikumbukwe kuwa alipoulizwa kuhusu nia yake ya kuunda kamati ya madini, Rais alisema kwamba alitaka kuzima “kelele za watu” wanaolalamikia mikataba ya madini na wanaodhani serikali yake imejaa ‘mijitu’ yenye kutaka kutumbua tu na kujishibisha bila kuwajali wananchi.

Hakika, hili la BoT ni kubwa zaidi, na limezua kelele nyingi zaidi. Hivyo, umma una kila sababu ya kuamini kwamba Rais amemfukuza Ballali (kivuli) ili kupoza hisia za wananchi na kutuliza kelele zao.

Lakini tusisahau kuwa wananchi wa leo wameshakomaa. Wanajua asili ya uchunguzi huu. Wanajua mengi kuhusu BoT. Wanatilia shaka kauli na vitendo vya serikali. Wanashangaa zaidi ujinga wa serikali (kutojua alipo mgonjwa wao) katika sakata la Ballali.

Wanapima umakini na uaminifu wa viongozi wao. Wanagundua kwamba linalofanyika sasa ni ‘sanaa’. Ni maigizo kama ya Ze Comedy! Yanafurahisha sehemu ya watazamaji, lakini wanajua kuwa ni maigizo tu; si maisha halisi.

Kinachoshangaza zaidi ni ile kauli kwamba Rais ameiagiza Takukuru na vyombo vingine kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua wahusika. Hii inazua maswali zaidi kwa sababu hatua za awali alipaswa kuzichukua yeye kama alivyofanya kwa Ballali.

Kwa nini uchunguzi mpya katika suala ambalo tayari limechunguzwa na matokeo yake ndiyo yaliyomfanya Rais ‘amfukuze’ Ballali? Kama uchunguzi huo ulikuwa wa maana kiutendaji, mbona Ballali amefukuzwa kabla ya uchunguzi huo (wa pili)?

Je, hao wengine waliotajwa katika ripoti ya wakaguzi, wameonewa kiasi cha serikali kutafuta njia ya kuwanusuru, tena kwa kuihusisha Takukuru ambayo imeshajizolea sifa ya kusafisha wakubwa na kuumiza walimu wa shule na mahakimu wadogo wadogo?

Kwa kuwa serikali imekataa kuweka ripoti hiyo ya BoT hadharani, hii ni njia nyingine ya kuwatoa kafara wachache na kuwalinda vigogo wanaotuhumiwa?

Lakini kinachotia kinyaa zaidi ni hicho kinachoitwa ‘rais ameagiza.’ Hivi Takukuru haiwezi kufanya kazi ya uchunguzi wa suala lililo wazi kama hili hadi iagizwe na Rais? Ndiyo, iko chini ya Ofisi ya Rais, lakini ina maana watendaji wake wanatenda kazi kwa amri ya Rais?

Je, haiwezekani amri hiyo hiyo ya Rais ndiyo itakayotumika kufukia mengine na kuibua mengine? Maana kama Takukuru ni ‘watiifu’ kwa Rais kwa viwango hivyo, Rais akikosea nao watakosea tu. Rais akipendelea nao watapendelea tu. Rais akionea mtu nao wanamwonea tu.

Maana yake, tunalazimishwa kudhani kwamba mkurugenzi wa Takukuru na watendaji wengine hawana kazi. Wanasubiri maagizo ya Rais. Hawana ujasiri wa kuchukua hatua dhidi ya watu walio karibu na rais, hata kama watagundulika ni mafisadi.

Hawana nguvu hata kidogo ya kufanyia kazi uchunguzi wao hadi kwanza ‘wamwonyeshe’ Rais uchunguzi wao, naye awaruhusu kumshitaki yeyote.

Kimsingi, suala hili halikupaswa hata kuibuliwa bungeni, bali Takukuru ilipaswa kuwa imeshalimalza siku nyingi na kuwapeleka wahusika wanakostahili kuwa.

Na hii si mara ya kwanza. Hata katika uchaguzi wa ndani wa CCM, ilisemekana Rais ndiye aliyeagiza Takukuru iwakamate waliokuwa wanatoa rushwa kununua uongozi, kana kwamba hiki ni chombo kisicho na watu walioajiriwa kwa kufuata taaluma zao.

Takukuru lazima wajue kuishi na kufanya kazi bila kutegemea maagizo ya Rais. Waamke usingizini, wafanye kazi zao bila kusubiri mambo yaibuliwe na ’wapinzani’ na wao waombe kuletewa ushahidi.

Maneno haya yanaudhi kweli. Lakini kinachopaswa kuudhi zaidi ni muundo na utendaji wa vyombo vyetu vya usalama.

Ukweli ni kwamba vipo kwa ajili ya watawala na ndugu zao, rafiki zao na maswaiba wao. Kama ambavyo nimekuwa nasema kila mara, usalama wa wananchi uko hatarini kila siku. Nguvu zote zinaelekezwa katika kulinda usalama wa wakubwa, hata kama ni wezi na mafisadi; hata kama ndio wanaodhuru usalama wa raia na taifa.

Hali hii inaendelea kusisitiza hoja ya wanaharakati tangu awali kwamba taasisi kama Takukuru inapaswa iwe huru; isiwe ofisini mwa Rais. Lakini kwa kuwa inawasaidia wakubwa kuonekana ‘wasafi’ na kwa kuwa chama chao kina wabunge wengi, hawataruhusu mabadiliko ya kisheria yanayoitoa Takukuru ofisini kwa Rais. Wanajua wanacholinda - ufisadi wa wakubwa!

Ndiyo maana nimekuwa nikisisitiza mara kwa mara kwamba Tanzania inahitaji mabadliko. Tuwe na watunga sheria wanaovuka mipaka ya vyama vyao; wanaolitazama taifa bila misingi ya kiitikadi.

Wingi wa wabunge wa CCM si neema kwa Watanzania. Ni ulinzi wa maovu ya wakubwa. Ni kitanzi cha wananchi maskini. Wingi wao ni kinga ya maovu ya wakubwa na ni mwendelezo wa sheria mbovu na katiba isiyojali matakwa ya wengi.

Ndiyo maana watu kama Ballali wanaweza kufanya lolote watakalo kwenye rasilimali zetu, wakajidai bila wasiwasi kwamba wana afya nzuri, wakakimbizwa na kufichwa nje ya nchi kabla mambo hayajawa mabaya; wakafichiwa siri hata wakiwa nje, na wakalindwa huko waliko ili wasirejee kutoboa siri za wakubwa.

Tukubali tukatae. Hili la Ballali nalo ni msumari mwingine katika kaburi la CCM ya awamu ya nne. Kadiri wanavyojaribu kuficha mambo, ndivyo mengine yanavyozidi kuibuka. Na haya hayakomi, hadi watawala wetu watakapotambua kuwa usanii si njia murua ya kuongoza taifa.

Napenda niwashauri viongozi wa serikali. Wawe wawazi na wakweli, hasa katika mambo yanayotuhusu. Na wanapotoa kauli, hata kama hawataki kusema ukweli, basi walau zifanane na ukweli.

Vinginevyo, nchi itaendeshwa kwa majungu, tetesi, uvumi huu na mwingine usiostahili kuandikwa hapa. Na haya mambo yatakapokuwa yamefikia kilele chake, mizizi ya uovu itakuwa imeota, na haitakuwa rahisi kuiong’oa. Nchi haitatawalika.

Viongozi makini lazima watazame mbali, wawe na mikakati ya muda mrefu kulinusuru taifa kutoka kwenye maangamizi yanayolikabili katika miongo michache ijayo.

Kwa sasa, katika utendaji wa serikali hii, siioni mikakati hiyo. Naona udhibiti wa matukio ya wakati huu. Naona kufukia fukia mashimo, kuziba watu midomo na kutuliza kelele – utendaji wa zima moto, miaka 46 baada ya uhuru! Bado tumekwama!

+447828696142
ansbertn@yahoo.com
www.ngurumo.blogspot.com


h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2008 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233  •  faksi +255-22-2126234  •  Selula  0713 296570