NIMESOMA taarifa ya TANESCO kujiondoa katika mkakati wa ununuzi wa mitambo ya Dowans, na nimeridhika kwamba ile inastahili kuitwa taarifa ya ‘mtajiju.’
Aya mojawapo ya taarifa hiyo iliyotolewa juzi na Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Dr. Idris Rashid inasema hivi: “Wananchi wa Tanzania watafanya maamuzi yao hapo ambapo nchi itakuwa imegubikwa na kiza, hospitali hazitoi huduma, viwanda havizalishi, wanafunzi vyuoni wanashindwa kusoma kwa sababu tulishindwa kufanya maamuzi.”
Huku ndiko kunaitwa kukata tamaa. Hapa kuna hasira. Kuna mkwamo wa mawazo unaozaa hitimisho la ‘mtajiju.’
Ni kielelezo cha mapenzi makubwa kati ya Serikali na Dowans, mapenzi yanayoipofusha Serikali na kuisahaulisha mgogoro kati yake na Dowans iliyofungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi, nchini Ufaransa.
Ni mapenzi yanayoshabihihana na yale yale ya vimemo vya wakubwa vilivyoipatia Richmond mkataba wa kuzalisha ‘umeme wa dharura’ ambao haikuzalisha, lakini ikalipwa mamilioni ya fedha zitokanazo na kodi ya wavuja jasho wa Tanzania.
Hii ni taarifa ya viongozi wanaonyanyua mikono. Wanataka kutuambia kwamba bila Dowans hakuna umeme; bila Dowans ni maafa. Tutawapuuza.
Haiingii akilini kwamba Serikali iliyoweza kuilipa Richmond sh milioni 152 kwa siku, haina pesa ya kununua mitambo mipya. Lakini ina sh bilioni 90 za kununua mitumba ya Dowans.
Hii ndiyo tafsiri yangu ya kauli ya Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, kwamba ni heri taifa kuingia gizani kuliko kununua mitambo ya Dowans!
Si kwamba anakata tamaa au halitakii mema taifa, bali ni kauli ya onyo, yenye kuonyesha ukali unaopinga kwa nguvu zote mikakati michafu ya mchakato wa Serikali kununua mitambo ya Dowans.
Ujumbe wa Dk. Mwakyembe ni kwamba tusitumie majanga ya kitaifa kama fursa za kuliibia taifa na kuwatisha wananchi kwa taarifa za kitaalamu zenye msukumo wa kisiasa.
Kwamba kama wapo waliowahi kudiriki kutuambia heri tule nyasi ili wakubwa washibe, basi sasa na sisi tuseme heri tukae gizani kuliko kuwaneemesha mafisadi. Ndivyo nilivyomtafakari na kumwelewa.
Mwakyembe anajua, na Watanzania wanajua, kuwa taifa haliwezi kuingia gizani eti kwa sababu mitambo ya Dowans haikununuliwa.
Ila anahisi kwamba inawezekana taifa likaingia gizani hata baada ya kununua mitambo ya Dowans. Si ni mitumba? Lolote linaweza kutokea.
Richmond imetufundisha. Hatuna sababu ya kuiamini Dowans. Wala Watanzania hawatajiju eti kwa vile TANESCO imejiondoa katika ununuzi wa mitambo hii.
Tunajua kwamba Serikali ina uwezo wa kupata mitambo mipya isiyo na utata. Tunajua kuwa ina uwezo wa kuandaa mipango mbadala. Lakini mipango hiyo haitaandaliwa iwapo tutawaruhusu kununua mitambo hii ya Dowans.
Na kwa wanaotazama mbele, hakuna haja ya kununua mitumba kama tuna uwezo wa kununua mitambo mipya. Zaidi ya hayo, Serikali inayojidai inapigana vita dhidi ya ufisadi, haina sababu ya kung’ang’ania mali iliyo na migogoro ya kifisadi.
Na iwapo tutakumbwa na giza, huko mbele ya safari, halitatokana na kushindwa kwetu kufanya uamuzi, bali kitakuwa kielelezo cha uamuzi mbovu wa watendaji serikalini.
Tukubaliane. Mitambo ya Dowans si mwokozi wa taifa. Hakuna mwenye uhakika kama mitumba hii ingeliepusha taifa na giza. Lakini tuna hakika kuwa ingetunisha mifuko ya wale wale tuliowanyang’anya tonge nono la Richmond.
Jeuri ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta, na wabunge wanaopinga jitihada hizi za Serikali, inatokana na ukweli wanaoujua kati ya Dowans na Richmond, na njama zinazofanyika kudhulumu Watanzania mamilioni mengine ya shilingi.
Wanajua kuwa ukombozi wa Tanzania hautegemei Dowans, wala hautatokana na mikakati ya zimamoto ya watawala.
Hatujasahau zimamoto ya iliyoileta Kampuni ya Net Group Solutions ya Afrika Kusini.
Bado tunakumbuka ahadi, sifa na mbwembwe kemkem; viboko na mitutu iliyowaingiza watendaji wa Net Group ofisini.
Tulikuja kusikitika baadaye tulipojua kuwa Net Group Solutions ilikuwa kampuni inayosemekana kuwa na ubia na familia ya Rais Benjamin Mkapa. Ni mradi mwingine wa vigogo ulioshindwa kuleta ukombozi ulioahidiwa.
Dhambi za Net Group Solutions na Richmond ndizo zimeutafuna mradi huu wa mitambo ya Dowans. Kumbukumbu bado ni mbichi. Wakubwa hawaaminiki.
Na ingawa Dk. Rashid anachukizwa na siasa kuingizwa kwenye suala analoita la utaalamu, ukweli ni kwamba anataka kufukia hoja kwamba hata wataalamu hao anaozungumzia, wanafanya kazi kwa kutumikia utashi wa kisiasa wa kundi jingine – kundi lisiloaminika!
Haliaminiki kwa sababu ya mwenendo wake wa kimaamuzi. Kama asemavyo mwanafalsafa Aristotle, sifa ya viongozi wetu haitokani tu na matendo yao bali tabia zao.
Kama ni matendo na mipango ya Serikali, ipo mingi. Lakini wananchi wanapima umakini wa mipango hiyo, wanatazama uwezo, nia na tabia ya viongozi wenyewe, wanaitilisha mipango hiyo.
Tabia za viongozi wetu na maswahiba wao ni kero mpya ya kitaifa inayojitokeza katika sura nyingi tofauti. Na ndiyo imefifisha kabisa imani ya wananchi kwa viongozi.
Hatuwezi kuirejesha imani hii kwa vitisho vya ‘mtajiju.’ Na katika hili la umeme, hatuwezi kuonyesha umakini wa mipango kwa kung’ang’ania mitambo chakavu.
Hata kama ingetusaidia leo, mitambo hiyo haiwezi kudumu kwa muda mrefu. Hivyo, tatizo la umeme halitakuwa limepatiwa ufumbuzi.
Sikitiko la baadhi ya wabunge na wananchi ni kwamba, miaka mitatu haijawatosha wenzetu kujifunza, kutulia na kutumia vizuri utabiri wa hali ya hewa kuweka mpango mkakati wa kuangamiza dharura hizi za umeme.
Wanafikiria tu umeme wa kuombea kura mwaka kesho. Baada ya hapo, hata kama taifa likiingia gizani wataishia kusema ‘mtajiju.’
Watakuwa wamepata wanachokitaka, na wengine watakuwa wanamalizia ngwe zao na kuwaachia warithi wao changamoto mbichi mbichi walizoahirisha kwa malengo ya kisiasa.
Kwa hiyo, hata isingekuwa ya Dowans, mitambo iliyotumika si suluhisho la matatizo ya umeme. Ni mitambo ya kuahirisha tatizo kwa muda. Na haya hayawezi kuitwa matokeo ya uamuzi wa kitaalamu.
Ni uamuzi wa zimamoto na siasa za kuahirisha matatizo. Lakini hatuwezi kuendekeza uongozi wa kuahirisha matatizo makubwa yanayolikabili taifa.
Watawala wanang’ang’ania mitumba kwa sababu na wao ni zao la siasa chakavu. Sasa watueleze. Wanakiri kwamba wanafanya siasa mitumba kwa sababu wao wameshakuwa mitumba ya kisiasa?