HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumapili, 5 aprili 2009
Yaliyopita
Pekua Tovuti
Wasiliana na Mwandishi
+447984584292
ansbertn@yahoo.comTuma barua-pepe
www.ngurumo.blogspot.comTembelea blogu
Siku 1,200 za urithi wa wizi na ubaguzi

Ansbert Ngurumo

 

RAIS Jakaya Kikwete amekaa madarakani kwa siku 1202. Amebakiza siku 625 kuondoka Ikulu. Lakini tayari chama chake kimeanza kampeni ya kumrejesha madarakani.

Na kampeni yenyewe imeanza kwa vitisho; tena vimeanzia ndani ya chama chake kuwatisha wanaowaza kuwania nafasi hiyo.

Wajuzi wa siasa za Tanzania, hasa ndani ya CCM, hawawezi kupuuza kauli za hivi majuzi za Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Samuel Malecela, na Katibu Mwenezi wa chama hicho, John Chiligati.

Wamesema kwamba wana CCM wanaowaza kuchukua fomu kuwania urais mwaka kesho wanajisumbua, kwa sababu mgombea wa CCM ni Rais Kikwete tu.

Wametoa na sababu, kwamba uongozi wake umeonyesha mafanikio makubwa sana; hivyo apewe nafasi nyingine.

Kwangu, kauli hizi ni zaidi ya maoni binafsi ya waliyotoa. Zina ujumbe wa chama; si wa Malecela wala Chiligati.

Hata zingekuwa zao binafsi, ni haki yao kutoa maoni kama wanachama wa CCM, lakini si haki yao kuingilia haki za wengine wanaotamani kuwania uongozi. Si sahihi kuwatisha!

Rais Kikwete mwenyewe hajasema kama anataka kugombea tena urais mwaka kesho. Kwa jinsi mambo yanavyokwenda, na kwa mtu makini, sidhani kama anafurahia kuendelea kukaa pale alipo.

Lakini hajakanusha kauli zao. Wamesema wazi na kusisitiza kwamba ndiye mgombea wao mwaka 2010. Amenyamaza. Ujumbe umefika. Hatutakosea tukisema anataka kuendelea.

Najua atakapoibuka mwaka kesho atatoa kauli za ‘milango iko wazi, anayetaka kugombea agombee.’

Lakini wanaojua siasa za CCM ni kwamba mlango umeshafungwa. Kufuli ni Malecela, na ufunguo ni Chiligati. Watakaojitokeza mbele ya safari watakuwa wasindikizaji ili kuhalalisha igizo la wakati huo.

Na ingawa siku 625 zilizobaki ni nyingi au chache kulingana na mtazamo wa mtu, tunajua kuwa hizo zitakuwa siku za maandalizi ya uchaguzi. Muda wa utumishi wao umekwisha. Kwa hiyo tuna haki ya kuwauliza maswali kuhusu utekelezaji wao wa ahadi za uchaguzi uliopita.

Tuchunguze ziara zao za kampeni ya 2005, hotuba zao na ahadi zao kila walikofika. Tulinganishe na siku walizokaa madarakani na walizobakiza. Tupime wameweza nini na wameshindwa nini.

Tuwahoji kama kwa kasi hiyo waliyotuonyesha wanastahili kupewa kura nyingine. Walituomba tuwape kura, tukawapa. Wakaomba muda, tukawapa.

Sasa tunahoji. Kwa muda huo wa siku 1202 tumevuna nini? Hiki tulichovuna (kama kipo) ndicho Malecela na Chiligati walitarajia? Kama wao wangepewa nafasi, ndicho wangetufanyia?

Na je, uwezo wa Malecela na Chiligati kupima mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne umekomea hapo? Na vipimo wanavyotumia kuipima serikali ndivyo vinavyotumiwa na Watanzania?

Lakini swali kubwa la leo, ambalo litaendelea kujitokeza mara kwa mara kwa staili tofauti, ni hili: kwa siku 1202, utawala wa Rais Kikwete umetuachia urithi gani?

Bahati nzuri ambayo pia ni mbaya, jibu la swali hili lilijulikana hata kabla serikali ya wanamtandao haijaingia madarakani.

Kashfa tunazosikia leo, za EPA na nyinginezo, zilifahamika mapema. Wahusika wa miradi feki na utapeli uliotumika kufadhili kampeni za uchaguzi ulioongeza nguvu za kuiweka serikali madarakani walifahamika mapema.

Mambo haya yalipokuja kuibuliwa kwenye mitandao ya intaneti na baadaye bungeni, watu walikuwa wanajaribu kupima kama wakubwa hawakuyajua au kama walikuwa na uwezo wa kujitenga, kuyakemea, kuyasitisha na kuchukua hatua.

Watanzania walipoanza kumhoji rais: ‘Utamfanyaje Rais Mkapa?’ walikuwa wanajua tuhuma zinazomkabili, na walitaka kupata kauli ya kiongozi mkuu wa nchi, ambaye naye alizijua kabla hajaingia madarakani.

Walitaka kujua dhamiri yake, nia yake, ujasiri wake na uwezo wake. Walitaka kumpima kama naye anachukia wizi uliotukuka ndani ya mfumo wa utawala wa nchi; kama ataendeleza urithi mbovu alioachiwa.

Baadhi ya wananchi waliamini kwamba hata kama naye ni zao la wizi huo, alikuwa na fursa ya kujitofautisha, kujitenga na wezi hao na kuchukua hatua dhidi yao, akafunga ukurasa huo na kufungua mwingine.

Wanaojua mwenendo wa mambo ndio wanaolalamika sasa kwamba hivi vijidagaa (kina Daniel Yona na Basil Mramba) si mifano tosha ya kuonyesha umakini na ukali wa serikali dhidi ya mafisadi.

Ndiyo hao wanaosisitiza kwamba mtu kama Andrew Chenge alipaswa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazoikabili serikali ya awamu ya tatu katika mikataba mikubwa ya wizi – kama ya rada na ndege ya rais.

Na wenye kutilia shaka uwezo na dhamira ya wakubwa, ndio wamekuwa wanashauri kwamba kama serikali iko makini na vita dhidi ya ufisadi, iiondoe taasisi ya kuzuia rushwa kwenye ofisi ya rais.

Inapokuwa chini ya ofisi ya rais, kama ilivyo sasa, utaona aibu kumtia rais na wapambe wake hatiani. Rais ndiye anakuwa bosi wa TAKUKURU. Ndiye anawanusuru na kuwatelekeza watuhumiwa. Hawezi kujikamata!

Kilichotokea katika sakata la uchunguzi wa mkataba wa Richmond ni sehemu ya ushahidi wa jitihada za TAKUKURU kuwabeba wakubwa. Nani atawaamini tena?

Kwa kushindwa kujitenga na wizi wa Awamu ya Tatu; na kwa kukataa kuchukua hatua kali dhidi ya watuhumiwa wakuu wa ufisadi wa awamu ya tatu; kwa kudumisha sheria, mila na desturi za utawala mkongwe uliochokwa na uliochukiwa na Watanzania, Rais Kikwete amejinyima fursa ya kuwa shujaa.

Amejitumbukiza katika matope ya wengine na amechafuka. Kibaya zaidi, amejinyima fursa ya kuweka na kung’oa mizizi ya wizi. Anatuachia urithi wa ufisadi.

Najua kuwa Mzee Malecela na mkewe Anne wanaishi nyumba moja. Ni wanachama na viongozi wa chama kimoja. Na niliwaona katika picha ya pamoja siku Anne alipokabidhiwa tuzo ya mwanamke jasiri iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani nchini kuthamini mchango wake katika kupambana na ufisadi.

Tuzo hiyo ina ujumbe wa ziada. Waliotoa tuzo wanaona uozo ndani ya chama na serikali. Wanajua hulka za watawala na wapambe wao. Wanajua nafasi ya Anne katika ulingo wa watawala.

Wanaona kwamba licha ya kivuli cha mumewe (Waziri Mkuu Mstaafu, Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu na Makamu Mwenyekiti wa CCM Mstaafu) ambaye pia ni mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu ya CCM, Anne ameweza kusema kile wanachoshindwa mamia ya wabunge wa CCM.

Ni ujumbe kwa wabunge wa CCM wanaokusanya posho za vikao na kuchangia kwa maandishi tu; wanaoogopa kusimama na kujitofautisha na wenzao; wasio tayari kuwaudhi wakubwa ili wasitemwe katika mchujo wa uongozi; wabunge ambao kwa kimya chao au kwa kuthubutu kuwanyamazisha wengine wanapalilia shamba la ufisadi wa wakubwa; wabunge wanaohujumu ustawi wa wananchi; wanaozungumza na kupamba lugha ya mafisadi; wabunge wanaopambana na wananchi!

Kama serikali ya Rais Kikwete ingefanya kazi yake vizuri tangu mapema, Anne Kilango Malecela asingepata tuzo hiyo. Angemkemea nani? Angemuumbua nani? Angemwadabisha nani? Angemkera nani?

Wananchi wanajua kwamba wakubwa serikalini hawapendi ‘kelele’ za Anne, lakini wakubwa hao hao wanafurahia vitisho vya Mzee Malecela.

Tuzo ya Anne ni ujumbe wa kidiplomasia wa serikali ya Marekani kwamba kuna tatizo kubwa ndani ya serikali yetu na kwamba watu wanaotoa kauli kama hii ya Mzee Malecela hawaisaidii jamii, na hawawezi kuipata tuzo hiyo.

Nakumbuka kwamba Mzee Malecela mwenyewe ni mwathirika wa urithi mwingine wa serikali ya awamu ya nne - ubaguzi.

Kama ilivyokuwa kwa Spika mstaafu Pius Msekwa, Malecela, alibaguliwa kwa umri wake kama ambavyo Dk. Salim Ahmed Salim alivyobaguliwa kwa nasaba yake. Wapo wengine walibaguliwa kwa makabila yao.

Ujasiri na uwazi uliotumiwa na wapambe wa Kikwete kusukuma hoja hizi kwa umma kupitia vyombo vya habari, ndiyo gundi inayopaswa kumfunga mdomo Mbunge wa Igunga na mpambe mkuu wa Kikwete, Rostam Aziz, linapozuka suala la ubaguzi wa aina yoyote. Hana uadilifu wa kulijadili.

Utamaduni wa kubaguana kwa viwango vilivyojitokeza mwaka 2005 ukiwahusisha hao hao wenye madaraka sasa, na wapambe wao, ni ugonjwa mkubwa unaoanza kuitafuna jamii yetu, na haukemewi kwa sababu waasisi wake ndio hao ambao wangeukemea.

Hakuna mtu anayetarajia Malecela au yeyote alipize kisasi cha kubaguliwa. Hana sababu. Na hana uwezo.

Lakini hakuna anayemtarajia pia asimame hadharani kupigia debe unyonge wa serikali, hasa anapokuwa karibu sana na moyo wa mwanamke jasiri kama mkewe, Anne.

Inawezekana Mzee Malecela ana busara nyingi, uzoefu mkubwa wa kisiasa, akili na elimu kuliko mkewe. Lakini katika hili la ujasiri, Anne Kilango Malecela analo la kumshauri mumewe.

Kwamba mambo yanapokuwa magumu kiasi hiki, kama na wewe si mmoja wa waasisi wa urithi huu wa wizi na ubaguzi, kuna mambo mawili unayoweza kufanya. Ama unakuwa jasiri unakemea waziwazi na kushauri vijana wako au unanyamaza kabisa ili usijihusishe na urithi huu mchafu.

Jambo moja liko wazi pia. Rais Kikwete anazo siku 625 za kufuta na kung’oa mizizi ya urithi huu wa wizi na ubaguzi. Kwa hili, tutampa muda kuanzia leo. Na akiliweza akaomba kuongezewa muda – kama bado anatamani kuendelea na adha ya Ikulu – hatutamkatalia. Akishindwa, wananchi watamhukumu.

Lakini kwa mambo yalivyo leo, kama hii ndiyo kazi kubwa inayosifiwa; na kama na yeye anaridhika na sifa anazopewa na kina Malecela, basi tumekwisha.

Kama rais hajatafsiri vema kauli zetu kwamba nchi inakabiliwa na ombwe la uongozi, na kama hafanyi lolote kuziba ombwe hilo, au kama anadhani ni yeye tu anayeweza kuliziba bila kubadilika, tumekwisha!



juu