SERIKALI sasa ipo njia panda kuhusu njia stahili inazopaswa izichukue kuhusu Kampuni ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI), inayojishughulisha na biashara ya kupanda na kuvuna pesa kinyume cha sheria.
Pamoja na serikali kubainisha kuwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Kifungu cha 171A, na kwa mujibu wa marekebisho ya sheria hiyo, kama yalivyofanywa na Sheria Na. 8 ya mwaka 2006, ni makosa ya jinai kwa mtu, kikundi au taasisi kuendesha biashara au shughuli yenye mfumo wa piramidi au upatu.
Licha ya ukiukaji wa sheria hiyo, bado serikali imekumbwa na kigugumizi cha kuchukua hatua kunakotokana na baadhi ya wananchi waliopanda mbegu (fedha) kudai kampuni hiyo ndiyo mkombozi wao kiuchumi, baada ya serikali kushindwa kuboresha maisha yao kama ilivyowaahidi katika ilani ya uchaguzi ya mwaka 2005.
Jambo jingine linaloifanya serikali iendelee kutafakari hatua za kuchukua zinatokana na idadi kubwa ya fedha walizowekeza baadhi ya wananchi ambao kwa takriban wiki moja sasa wamekuwa wakijazana katika ofisi za DECI kupanda na kuvuna fedha zao.
Taarifa mbalimbali zinaeleza kuwa kampuni hiyo ina wanachama wasiopungua 700,000, ambao nyuma yao kuna watu wasiopungua milioni 3.5.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari kilichozungumza na Tanzania Daima Jumapili, kimedai kuwa iwapo serikali itachukua hatua za kuifunga au kukamata baadhi ya watendaji wa DECI, kuna kila dalili za kutokea kwa vurugu miongoni mwa jamii.
Chanzo hicho kimebainisha kuwa kwa hali ilivyo hivi sasa, suala hilo limeingizwa kidini na kisiasa, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limezidisha ugumu wa kulitatua.
Tamko la maaskofu zaidi ya 30, wa Kanisa la Pentekoste, walilolitoa hivi karibuni la kuwataka Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuingilia kati kuinusuru kampuni hiyo, kwa kile walichodai kuwa iweze kuendelea na kazi yake ya kuondoa umaskini kwa Watanzania, limeonyesha mizizi ya DECI ilianza kazi mwaka 2007.
Tamko hilo ambalo pia lilikuwa na tishio kuwa iwapo kampuni hiyo haitaruhusiwa kufanya shughuli zake, basi wapiga kura katika uchaguzi wa mwaka 2010 watachagua pumba na mchele.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wametafsiri kauli hiyo kama ni tishio kwa serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo katika uchaguzi mkuu uliopita ilishinda kwa kishindo.
Wakati viongozi wa dini hao wakiitetea DECI, serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, amesisitiza kuwa wananchi wanaoweka fedha zao katika kampuni hiyo wanahatarisha mitaji yao na kuitaka DECI kama inataka kufanya shughuli wanazozifanya sasa wafuate taratibu.
Taarifa hiyo ya serikali iliwafanya baadhi ya watu waliopanda mbegu zao kwenda katika ofisi za kampuni hiyo kwa lengo la kuchukua fedha zao, lakini uongozi uligoma kuwapa kwa madai kuwa muda wa kuvuna fedha hizo bado haujafika.
Pia uongozi huo wa DECI juzi na jana ulitoa matangazo mbalimbali katika vyombo vya habari wakidai fedha za waliopanda mbegu zipo salama na wanafanya utaratibu wa kufuata sheria ili waweze kufanya shughuli zao bila bughudha.
Tahadhari za serikali kwa wananchi kuhusu DECI zinadaiwa zilifanywa na mmoja wa raia mwema ambaye aliandika barua pepe kwenda kwa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana nchini (CMSA), akieleza kuwa kampuni hiyo inaendesha biashara haramu kwa mfumo unaoitwa piramidi au upatu.
Kwa mujibu wa barua pepe hiyo, Kampuni kama DECI iliyojulikana kwa jina la PONZI, ilikufa huko nchini Kenya mwaka 2007, baada ya wanachama wenye hasira kumrusha meneja wa lililokuwa tawi la kampuni hiyo jijini Nairobi, kutoka ghorofa ya nane, pale walipogundua kuwa fedha zao zimepotea kwenye mfumo huo wa piramidi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Soko la Mitaji na Dhamana (CMSA), Dk. Fratern Mboya, Septemba 12, 2008, alitoa taarifa rasmi kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Jeshi la Polisi Makao Makuu, kuwa Kampuni ya DECI (T) Ltd inaendesha biashara haramu yenye mfumo unaoitwa piramidi au upatu.
Pamoja na barua hiyo, inadaiwa hakuna juhudi za dhati kuizuia DECI isifanye shughuli zake jambo lililofanya kampuni hiyo ipanue zaidi shughuli zake na kuwahusisha watu wengi zaidi.
Aidha, taarifa za kuaminika kuhusu uchunguzi uliofanywa na kitengo cha kuzuia fedha haramu cha Kurugenzi ya Makosa ya Jinai, ndani ya Jeshi la Polisi nchini, zilieleza kuwa DECI ilisajiliwa nchini na Msajili wa Makampuni (BRELA), mwaka 2007, na kupewa namba ya usajili 61334.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, DECI ilianzishwa na wakurugenzi wanne, majina tunayo, watatu kati ya hao wakiwa na hisa ya asilimia 10 kila mmoja, na mwingine mmoja akiwa na hisa ya asilimia 20.
Zilieleza kuwa asilimia hamsini ya hisa iliyobaki, inamilikiwa na Kanisa la Jesus Christ Deliverance of Tanzania.