MAJINA ya wamiliki wa Kampuni ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI), inayojishughulisha na biashara ya kupanda na kuvuna pesa, sasa yamebainika.
Hata hivyo, uraia wa wamiliki hao bado haujajulikana vema baada ya wote kuonekana kuwa na majina yenye asili ya makabila ya nchini Kenya.
Vyanzo vyetu vya habari viliwataja wamiliki (wakurugenzi) hao wa DECI na hisa wanazomiliki kwenye mabano kuwa ni Mchungaji Jackson Sifaeli Mtaresi (hisa asilimia 20), Mchungaji Dominick Kigendi (asilimia 10), Timotheo ole Loitinng’ye (asilimia 10) na Samweli Safaeli Mtaresi (asilimia 10).
Kwa mujibu wa habari hizo, mmiliki mwingine mkubwa wa DECI ni Kanisa la Jesus Christ Delivarence of Tanzania, ambalo linamiliki asilimia 50 ya hisa, hivyo kukamilisha asilimia 100 ya hisa za kampuni hiyo iliyozua mjadala nchini.
Habari zaidi zilisema kuwa, kati ya wamiliki hao, walio na mamlaka ya kuidhinisha fedha za DECI (signatories), ni Mchungaji Kigendi na Loitinng’ye.
“Mchungaji Kigendi na Ole Loitinng’ye, ndio wenye mamlaka ya kusaini fedha, ila uraia wa watu hawa bado hatujaujua, lakini kama mnavyoona, majina yao yanaonekana kuwa na asili ya makabila ya nchini Kenya,” alithibitisha ofisa mmoja serikalini, ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Taarifa zaidi kutoka Kitengo cha Uchunguzi wa Fedha Haramu, zinaonyesha kuwa, wakurugenzi wawili wa kampuni hiyo, wana akaunti zenye majina yao binafsi kwenye benki ya BOA, tawi la Sinza, jijini Dar es Salaam, zenye zaidi ya sh bilioni moja kila moja, fedha ambazo sehemu yake zilitumika katika mchakato wa uanzishaji wa kampuni hiyo.
Wakurugenzi hao ambao akaunti zao tumezihifadhi kwa sasa ni Mchungaji Kigendi na Mchungaji Loitinng’ye.
“Kitengo cha Kupambana na Fedha Haramu cha Wizara ya Fedha na Uchumi kinachoitwa “Financial Intellegence Unit”, kilimwandikia barua Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Jeshi la Polisi, kikimjulisha kuwepo kwa taarifa kutoka Bank of Afrika (BOA), kuhusu hamisho la fedha nyingi la sh bilioni moja, kutoka kwa Mchungaji Ole Loitinng’ye (Mkurugenzi wa Kampuni ya DECI (T)) kwenda kufungua akaunti mpya ya Kampuni ya DECI (T) Ltd.,” kilisema chanzo chetu kutoka kwenye kitengo hicho.
Aidha, imebainika kuwa ufunguzi wa akaunti ya DECI, yenye fedha zaidi ya sh trilioni 1, ulifanyika kutokana na ushawishi wa Jeshi la Polisi, baada ya kugundua wakurugenzi wa kampuni hiyo, wanaweka fedha nyingi kwenye makasha ndani ya maofisi ya matawi yao au majumbani mwa viongozi wa kampuni hiyo.
Sakata la DECI inayoendesha shughuli zake kwa miaka mitatu sasa nchini, lilianza baada ya raia mwema mmoja, jina tunalo, kufichua siri ya kampuni hiyo, kupitia barua pepe aliyoiandika kwa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana nchini (CMSA), akieleza wasiwasi wake kuwa kampuni hiyo inaendesha biashara haramu kwa mfumo unaoitwa piramidi au upatu.
Kwa mujibu wa barua pepe hiyo, kampuni inayofanana na DECI iliyojulikana kwa jina la PONZI, ilikufa huko nchini Kenya mwaka 2007, baada ya wanachama wenye hasira kumrusha meneja wa lililokuwa tawi la kampuni hiyo jijini Nairobi, kutoka ghorofa ya nane, pale walipogundua kuwa fedha zao zimepotea kwenye mfumo huo wa piramidi.
Sehemu ya barua pepe hiyo kwenda kwa CMSA, ambayo Tanzania Daima inayo nakala yake, raia mwema huyo aliandika hivi;
“Wapendwa CMSA, hivi punde nimegundua kuna kampuni ya kutia shaka inayoendesha shughuli zake hapa Dar es Salaam. Kampuni hiyo inaitwa DECI Tanzania Limited. Wana ofisi yao katika ghorofa ya pili ya jengo la Mwanamboka, eneo la Kinondoni, Manyanya. Pia kwa mujibu wa nakala yao ya viwango vya fedha, inaonesha pia wana ofisi nyingine eneo la Mabibo Mwisho. Utaweza kuona baadhi ya namba za simu na anuani pepe zilizoainishwa kwenye karatasi hiyo.
“Wanawadanganya watu ambao hawajashituka, kwa maneno ya kuvutia, kwamba ‘tulianza kwa kuwasaidia wachungaji na wainjilisti kueneza neno la Mungu, lakini Serikali ya Tanzania na BoT, wametuomba tupanue huduma zetu kuwasaidia watu wote, bila kujali dini’. Wanawaambia watu kwamba wamepewa leseni na BoT inayowaruhusu kuchukua amana.
“Kwa kuwa naifahamu Taasisi ya PONZI ya Kenya, na kwa kuwa DECI inaonekana kuwa kama hiyo, nashauri muichunguze na kuutaarifu umma.”
Septemba 12, 2008, Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Dk. Fratern Mboya, alitoa taarifa rasmi kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Jeshi la Polisi Makao Makuu, kuwa Kampuni ya DECI, inaendesha biashara haramu yenye mfumo unaoitwa piramid au upatu.
Sehemu ya barua ya CMSA yenye kumbukumbu namba, CMSA/F3/B4/49, ya Septemba 11, 2008, kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa Makosa ya Jinai, na ambayo tunayo nakala yake, ilisema hivi;
“Kufuatia taarifa kutoka kwa watu binafsi kuhusu Tanzania Care Revolving Fund (DECI), kichwa cha habari hapo juu chahusika. Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) inaona kuwa DECI inaendesha mfumo unaoitwa ‘vuna kutokana na mbegu uliyopanda’, ambapo ni kinyume cha Sheria ya Kanuni za Adhabu (Sura ya 16). Kwa mujibu wa sheria hiyo, ‘vuna kutokana na mbegu uliyopanda’, ni mchazo haramu wa piramidi.”
Kwamba, kwa mujibu wa Sheria na Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Kifungu cha 171A, na kwa mujibu wa marekebisho ya sheria hiyo, kama yalivyofanywa na Sheria Na. 8 ya mwaka 2006, ni makosa ya jinai kwa mtu, kikundi au taasisi kuendesha biashara au shughuli yenye mfumo wa piramidi.
Kupitia barua hiyo, CMSA iliomba msaada wa Jeshi la Polisi, kufanya upelelezi na utekelezaji wa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi na sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana.
“Kwa kuzingatia vigezo hivi na kutekeleza jukumu kubwa la kulinda maslahi ya wawekezaji katika biashara ya masoko ya mitaji, CMSA inaomba msaada wa Jeshi la Polisi ili kufanya upelelezi na utekelezaji wa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi na sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana,” ilihitimisha barua hiyo.
Aidha, taarifa za kuaminika kuhusu uchunguzi uliofanywa na Kitengo cha Kuzuia Fedha Haramu cha Kurugenzi ya Makosa ya Jinai, ndani ya Jeshi la Polisi nchini, zilieleza kuwa DECI ilisajiliwa nchini na Msajili wa Makampuni (BRELA), mwaka 2007, na kupewa namba ya usajili 61334.
Uchunguzi huo pia ulibaini kuwa, kampuni hiyo ina zaidi ya matawi 46 nchi nzima, pamoja na washiriki zaidi ya 430,276, lakini pamoja na kuwa na matawi yote hayo, ina akaunti moja tu, iliyopo jijini Dar es Salaam, kwenye benki ya BOA, tawi la Sinza, ambayo ina kiasi cha sh trilioni 1.038.
“Utaratibu wa kujiunga kuwa mshiriki wa TRF ni lazima mwombaji awe Mtanzania mwenye kitambulisho cha kupigia kura, kutoa ada ya kiingilio ambayo ni sh elfu ishirini, inayotolewa mara moja na baada ya hapo mwombaji anatakiwa kujaza fomu iitwayo White Card. Baada ya kutekeleza hayo, mwanachama anaweza kuweka fedha au kupanda mbegu kulingana na uwezo wa mshiriki,” ilieleza taarifa hiyo.
Upandaji huo wa mbegu una viwango vyake ambapo kiwango cha chini ni sh 10, 000, kiwango cha kati sh 20, 000 mpaka 100,000, na mpandaji hutakiwa kuvuna baada ya majuma manane (miezi miwili).
Kiwango cha juu ni sh 200,000, ambapo mpandaji hutakiwa kuvuna sh 500, 000, baada ya majuma 17.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, hadi sasa jeshi lake haliwezi kusema chochote kwani kuna kamati iliyoundwa kwa ajili ya kushughulikia suala hilo na bado inaendelea na kazi yake.