HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumanne, 14 aprili 2009
Yaliyopita
Pekua Tovuti
DECI Kampuni inayowaliza wachungaji, wateja

Asha Bani

 

KATIKA kuhakikisha kila Mtanzania anajikwamua katika lindi la umaskini, kila kukicha kumekuwa na mbinu mbalimbali zinazobuniwa na wananchi ili kuweza kujipatia kipato cha kila siku.

Mara kadhaa mbinu zinazobuniwa na wananchi zinatakiwa ziwe halali ili zisilete migongano na taasisi au serikali inayotakiwa kuihalalisha kampuni husika.

Hivi karibuni serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ilitangaza kuwa kampuni ya Entreprenuership for Community Initiative (DECI) inayofanya kazi ya upatu maarufu kama ‘Kupanda na Kuvuna,’ kuwa ni batili kutokana na kubaini inafanya kazi hiyo bila kufuata taratibu za kisheria ya kutoa mikopo nchini.

Taarifa ya kutahadharishwa kwa wananchi kuhusu DECI ilitolewa na Gavana wa BoT Profesa Benno Ndulu na Dk. Fratern Mboya Mkurugenzi Mtendaji wa CMSA, kuwa wao wasijelaumiwa pindi matatizo yakijitokeza kuhusiana na kampuni hiyo ambayo haina leseni ya kuendesha shughuli hizo.

Kutangazwa kwa taarifa hiyo na serikali iliwashtua wengi ambao kwa upande wao wamejiunga na kuendela kuvuna kwa kipindi cha miaka mitatu sasa tangu kuanzisha kwa DECI.

Baadhi ya watu walioshangazwa hadi kufikia hatua ya kutoa tamko rasmi kwa serikali ni wachungaji na waumini wa makanisa mbalimbali nchini wakiongozwa na Askofu na Mwenyekiti wa Makanisa ya Pentekoste nchini, Sylivester Gamanywa.

Wachungaji hao walitoa tamko lao likiambatana na kutoa ushuhuda kwamba DECI imewanufaisha kwa namna moja ama nyingine huku wachungaji wengine wakidai wamejenga nyumba na kununua magari kutokana na DECI.

Ushuhuda wa maaskofu ulifanyika katika Viwanja vya Sabasaba, Dar es Salaam, ambapo kulifurika maelfu ya wateja wakiwa hapo bila kujali mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha.

Akizungumza katika eneo hilo Mchungaji Batholomeou Sheggah ameitaka BoT kuacha kuiingilia kati kampuni hiyo kwani imewanufaisha sana.

Mbali na kuitaka BoT kutoingilia kampuni pia amemtaka Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuingilia kati ili kuinusuru DECI.

Kwa wakati tofauti walitoa ushuhuda wao huku Mchungaji Sheggah akidai amenufaika na DECI kupitia mambo mbalimbali ikiwemo kujenga kanisa na hata kununua gari tofauti na zamani alipokuwa akitembea bila ya usafiri.

‘‘DECI imeninufaisha sana kwa kuwa nilikuwa natembea kwa kutumia miguu lakini kwa sasa natembea kwa kutumia usafiri wangu... DECI imeninufaisha kweli naiomba serikali iingilie kati ili kuhakikisha kuwa inafanyiwa taratibu zote na kuendelea na shughuli zake,” anasema Sheggah.

Anasema, anaishangaa BoT ‘kuikalia,’ barua yao ya maombi ya kutaka kupatiwa usajili ambapo hadi leo kuna maombi mbalimbali yametumwa kwao.

Sheggah anasema kukaa kimya kwa BoT kunaashiria kuwa wamekubaliwa na kama watachukua jukumu la kuifungia, yeye (Sheggah) atakwenda mahakamani tena yeye atasimamia kesi hiyo kama wakili.

Mara baada ya tamko hilo kutolewa na wachungaji, baadhi ya wachunguzi wa mambo mbalimbali nchini walibaini kuwa DECI ilianzishwa nchini mwaka 2007, baada ya kampuni yenye mfumo kama huo kufa huko nchini Kenya na kuwadhulumu maelfu ya wanaupatu wake waliojiunga nayo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyoandikwa na gazeti Tanzania Daima wiki iliyopita kampuni hiyo inaendesha biashara haramu kwa mfumo unaoitwa piramidi au upatu.

Kwa mujibu wa barua pepe hiyo, kampuni kama DECI iliyojulikana kwa jina la PONZI, ilikufa huko nchini Kenya mwaka 2007, baada ya wanachama wenye hasira kumrusha meneja wa lililokuwa tawi la kampuni hiyo jijini Nairobi, kutoka ghorofa ya nane.

Kurushwa kwa meneja huyo kunatokana na wateja wa upatu huo kujua kuwa fedha zao zimepotea kwenye mfumo huo wa piramidi jambo ambalo lilizua utata mkubwa.

Barua hiyo iliandikwa hivi “Wapendwa CMSA, hivi punde nimegundua kuna kampuni ya kutia shaka inayoendesha shughuli zake hapa Dar es Salaam. Kampuni hiyo inaitwa DECI Tanzania Limited. Wana ofisi yao katika ghorofa ya pili ya jengo la Mwanamboka, eneo la Kinondoni, Manyanya.

‘‘Kwa mujibu wa nakala yao ya viwango vya fedha, inaonyesha pia wana ofisi nyingine eneo la Mabibo Mwisho. Utaweza kuona baadhi ya namba za simu na anuani pepe zilizoainishwa kwenye karatasi hiyo…

“Wanawadanganya watu ambao hawajashtuka, kwa maneno ya kuvutia, kwamba ‘tulianza kwa kuwasaidia wachungaji na wainjilisti kueneza neno la Mungu, lakini Serikali ya Tanzania na BoT, wametuomba tupanue huduma zetu kuwasaidia watu wote, bila kujali dini.

‘‘Wanawaambia watu kwamba wamepewa leseni na BoT inayowaruhusu kuchukua amana…

“Kwa kuwa naifahamu taasisi ya PONZI ya Kenya, DECI inaonekana kuwa kama hiyo, nashauri muichunguze na kuutaarifu umma.”

Septemba 12, 2008, Dk. Fratern Mboya wa CMA , alitoa taarifa rasmi kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Jeshi la Polisi Makao Makuu, kuwa Kampuni ya DECI (T) Ltd inaendesha biashara haramu yenye mfumo unaoitwa piramidi au upatu.

Sehemu ya barua ya CMSA yenye kumbukumbu namba CMSA/F3/B4/49, ya Septemba 11, 2008, kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa Makosa ya Jinai, ambayo nakala ya barua hiyo Tanzania daima inayo inaeleza hivi:

“Kufuatia taarifa kutoka kwa watu binafsi kuhusu Tanzania Care Revolving Fund (DECI), kichwa cha habari hapo juu chahusika. Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) inaona kuwa DECI inaendesha mfumo unaoitwa “Vuna kutokana na mbegu uliyopanda,” ambapo ni kinyume cha Sheria ya Kanuni za Adhabu (Sura ya 16). Kwa mujibu wa sheria hiyo, ‘Vuna kutokana na mbegu uliyopanda’, ni mchezo haramu wa piramidi,”.

Hata hivyo kwa mujibu wa Sheria na Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Kifungu cha 171A, kwa mujibu wa marekebisho ya sheria hiyo, kama yalivyofanywa na Sheria Na. 8 ya mwaka 2006, ni kosa la jinai kwa mtu, kikundi au taasisi kuendesha biashara au shughuli yenye mfumo wa piramidi.

“Kwa kuzingatia vigezo hivi na kutekeleza jukumu kubwa la kulinda maslahi ya wawekezaji katika biashara ya masoko ya mitaji, CMSA inaomba msaada wa Jeshi la Polisi ili kufanya upelelezi na utekelezaji wa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi na sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana,” ilihitimisha barua hiyo.

Hata hivyo DECI imekuwa kama kizungumkuti ambacho kinazua utata mkubwa huku wakiwa hawajakamilisha taratibu zake lakini pia inadaiwa ilipatiwa usajili wake na Msajili wa Makampuni (BRELA), mwaka 2007, na kupewa namba ya usajili 61334.

Habari zingine zilizotoka katika vyombo vya habari zilizeleza kuwa hivi karibuni siri ziliendelea kuvuja kuhusu kampuni hiyo ambapo wahasibu wa mashirika ya umma wanadaiwa kuchota mafungu ya fedha kwa lengo la kuvuna katika DECI.

Kufuatia hali hiyo inasadikiwa kuwa watumishi wa umma mbalimbali wana wasiwasi mkubwa wa kuburutwa mahakamani pindi watakapofanyiwa uchunguzi na Jeshi la Polisi nchini.

Jwa sasa macho ya Watanzania walio wengi yako kwa wateja wa DECI huku wachungaji wakisubiri kujua nini kitafuata na ni nini tamko la serikali kuhusiana na tuhuma hizo zinazoelekezwa kwa DECI.

Utaratibu wa DECI ni pamoja na kuwa na kiingilio cha sh 20,000 inayotolewa mara moja na baada ya hapo mwombaji anatakiwa kujaza fomu iitwayo ‘White Card’.

Baada ya kutekeleza hayo, mwanachama anaweza kuweka fedha au kupanda mbegu kulingana na uwezo wa mshiriki.

Katika upandaji huo wa mbegu kuna viwango vyake ambapo kiwango cha chini ni sh 10,000, kiwango cha kati sh 20,000 mpaka 100,000, na mpandaji hutakiwa kuvuna baada ya majuma manane (miezi miwili).

Kiwango cha juu ni sh 200,000, ambapo mpandaji hutakiwa kuvuna sh 500,000, baada ya majuma 17.

Katika kiwango cha chini ambacho ni sh 10,000, mpandaji huvuna sh 25,000, lakini wakati wa kuvuna ile sh 10,000 itaendelea kubaki DECI (T), kama mbegu na kinachobaki hukatwa asilimia 15, ambayo hubakia kwenye kampuni hiyo, kwa shughuli za ofisi.

DECI imetengeneza ajira za watu wapatao milioni mbili kwa kutoa huduma katika mikoa 17 na kuwa na matawi 36 nchini kote ambapo inahudumia watu milioni 3.5 .

Hata hivyo mara nyingi wakurugenzi wa DECI wanapotafutwa katika simu ili kutolea ufafanuzi suala hilo huwa wanakata simu ama kwa maana nyingine wanadai kuwa hawawezi kuongelea suala hilo kwa kuwa ni mapema mno na bado utaratibu unafuatwa kuhusiana na kutafuta kibali cha kuendesha shughuli hizo.



juu