HATIMAYE Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, amewataja kwa majina watuhumiwa watano wa ufisadi kati ya kumi aliowaita kuwa ni ‘mafisadi papa’, walioshindikana kuchukuliwa hatua.
Mengi ambaye amekuwa kinara wa mapambano dhidi ya ufisadi hadi kupata tuzo ya heshima ya Martin Luther King, aliwataja kwa majina mafisadi hao katika mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika ofisini kwake, jijini Dar es Salaam, jana.
Kati ya mafisadi hao aliowataja, wamo wafanyabiashara wanne wenye asili ya Kiasia na mbunge mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), anayetoka Kanda ya Magharibi ambao majina yao tunayo, lakini hatuwezi kuyataja kwa sasa.
Mengi alisema mafisadi hao wanaotuhumiwa kuiba mabilioni ya fedha za wananchi, lazima washughulikiwe kwa ujasiri kwani wanaogopwa kutokana na uwezo wao kifedha.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa, watuhumiwa hao, wenye fedha nyingi, wanahusishwa na kashfa karibu zote nchini, ikiwamo mikataba ya kampuni za kufua umeme wa dharura - Richmond na Dowans, wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), ununuzi wa helikopta na magari ya jeshi, ndege ya rais, uuzaji wa majengo ya NSSF, NSPF, uendeshaji wa Bahati Nasibu ya Taifa, mradi wa mkaa wa mawe wa Mchuchuma na kashfa nyingine nzito.
Alisema mafisadi hao, wamefikia hatua ya kupambana na watu wachache waliojitoa mhanga kupinga masuala ya ufisadi nchini.
“Nchi imekumbwa na ufisadi na kusababisha iingie katika mtafaruku mkubwa kutokana na mafisadi kutotaka kuguswa.
“Mafisadi Papa, wamecharuka na kufikia hatua ya kupambana na wote wanaomsaidia Rais Jakaya Kikwete kupambana na ufisadi kwa kuwazuia wasiendelee kuitafuna nchi,” alisema Mengi.
Hata hivyo, Mengi amewatahadharisha mafisadi hao kuwa lazima wajue kwamba iwapo wapambanaji wa ufisadi watapatwa na madhara, iwe kuuawa kwa sumu kwenye chakula ama ajali, wataulizwa na Watanzania, na watawajibishwa kwa matendo yao.
“Kutokana na kujulikana kwa majina, wanaweza kuua hata kama upo nje ya nchi, hawa wana pesa nyingi, wanaweza kuajiri mtu kukuua, si lazima uuawe nchini, hata nje ya nchi, ilimradi wapoteze ushahidi,” alisema Mengi.
Alisema mafisadi, wamesababisha Watanzania kutumia muda mwingi kujadili masuala ya ufisadi badala ya maendeleo ya nchi hii na mambo mengine ya msingi.
“Mafisadi papa, hawatuibii rasilimali tu, wanatuibia pia muda, badala ya kutumia muda wetu katika shughuli za maendeleo, tunajikuta tunatumia muda mwingi kupambana nao na wala hawatingishiki.
“Wanatumia fedha walizotuibia kutudharau, kututukana na kutunyanyasa, wanaendelea kutumia uwezo wao wa kiuchumi uliotokana na wizi wa rasilimali za nchi yetu, kushawishi na kupata miradi mikubwa mikubwa kwa kutumia majina tofauti tofauti, huku wakipuuza kelele za wananchi kuhusu ufisadi.
“Ni lazima Watanzania sasa tujiulize, hivi hawa mafisadi wanapata wapi ujasiri wa majigambo, dharau na nguvu za kututukana na kutunyanyasa? Ni lazima tuone kwamba sasa tumefika mahali pa kusema imetosha! ‘Enough is enough’,” alisema Mengi.
Alisema watuhumiwa hao hata kama wakiamua kumfikisha mahakamani, yeye hajali na badala yake atafurahia hatua hiyo.
“Waende mahakamani, tena kesho (leo), pamoja na pesa zao hawawezi ku-influence mahakama, wakiamua kunifikisha katika vyombo vya sheria sawa, nitafurahi kwa sababu karibu kila kashfa kubwa wapo wao.
“Tena mahakamani tutayajua mengi zaidi, huu ni mfano tu, mahakama inatenda haki. Unajua hawa jamaa (mafisadi) wanataka tuwe kama kondoo, yaani wakikwambia weka shingo tukuchinje ukubali na ukikataa wanapiga kelele,” alisema Mengi.
Alisema endapo watuhumiwa hao watashughulikiwa kisheria, waliosalia wataisha na hatimaye ufisadi kutokomea nchini.
‘‘Siku zote huwezi kumaliza suala la rushwa kwa kumshughulikia yule anayepokea rushwa, kuna wengine wanapokea kwa kulazimishwa, kama fisadi papa mmoja anaweza kutoa rushwa kwa watu 1,000 ukimshughulikia yeye mtoaji, hakika waliobaki hawatapata rushwa na hatimaye kuisha.
“Mafisadi papa tukiwaweka pembeni kwa muda, vita dhidi ya ufisadi itafanikiwa, lakini tukiwaacha utakuwa kama mchezo wa kuigiza.
“Watanzania wanapata shida sana, mimi mwenyewe nimetoka katika umaskini...ni lazima tukumbuke tulipotoka, kwani kila anayemtetea fisadi anasaliti yule maskini aliyemuacha kijijini, ambako shule hazina madawati, hospitali hazina dawa.
“Tukumbuke hata tukiwasaliti tutarudi kule kule kijijini kuzikwa, tena na wale wale ambao leo hawana chakula, tena tutazikwa huku nguo zao zikiwa zina viraka,” alisema.
Alisema inavyoonekana mafisadi papa wanataka kuvuruga nchi, na si ajabu wakaunga mkono suala la Kampuni ya Entreprenuership for Community Initiative (DECI) na Watanzania wakabaki kufukuzana na wachungaji bila kujiuliza ni kina nani hasa wanachochea.