HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumapili, 26 aprili 2009
Yaliyopita
Pekua Tovuti
Wasiliana na Mwandishi
+447984584292
ansbertn@yahoo.comTuma barua-pepe
www.ngurumo.blogspot.comTembelea blogu
Mengi anamsaidia Rais Kikwete?

Ansbert Ngurumo

 

MAMBO mawili makuu yaliyotawala mjadala katika vyombo vya habari wiki hii ni dhihaka ya wasanii kwa Rais Jakaya Kikwete na ‘mlipuko’ mzito wa kauli ya Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, dhidi ya wale aliowaita mafisadi papa – na akataja watano tu.

Yote mawili yametugawa. Katika tukio la kwanza, (mtu anayefanana na kiongozi wa serikali alichorwa na kudhihakiwa kwenye mtandao mmoja wa intaneti uliojaa vituko, unaoendeshwa na watu ambao bado hawajafahamika).

Kwa upande wake, Mengi amewataja na kuwatuhumu watu wazito watano, mbele ya vyombo vya habari, kwa msisitizo mkubwa mno uliozusha mjadala mpya katika jamii na kuibua maswali kadhaa yanayoendelea kujadiliwa.

Mambo haya mawili yamewafanya baadhi ya wananchi kusema kwamba haya ni matumizi mabaya ya vyombo vya habari.

Wanadai si sahihi watu kumdhihaki kiongozi wa taifa kwa sababu, naye ni mkuu wa nchi anayebeba taswira ya nchi; na si vema kabisa kwa mtu anayemiliki vyombo vya habari kuvitumia kutangaza tuhuma nzito dhidi ya watu wengine.

Hata hivyo, nadhani wapo wanaoamini kwamba kwenye siasa, dhihaka hunoga pale inapowagusa wakubwa. Na hapo ndipo pake.

Na ingawa wamejitokeza baadhi ya watu kudai kwamba taarifa ya Mengi haikuwa habari kwa sababu majina yale si mageni, yalishatajwa na yanafahamika tu, habari ni kwamba Mengi naye ameingia katika orodha ya wanaotaja mafisadi hadharani, bila woga.

Na habari hii inakuzwa pia na ukubwa, jeuri na hata ‘umafia’ wa mafisadi wenyewe. Wasifu binafsi wa Mengi na mafisadi husika, tukio husika na ujumbe uliomo ndiyo habari yenyewe.

Wala haya si matumizi mabaya ya vyombo vya habari. Navitetea. Nawatetea na wanaovitumia. Najua nitazusha utata na matata. Lakini maelezo yapo.

Hoja yangu kuhusu dhihaka kwa kiongozi wa taifa ni moja na fupi tu. Kwanza, hakuna anayeweza kuthibitisha kwamba picha iliyokuwa kwenye mtandao ni ya kiongozi wetu. Anaweza kuwa mtu mwingine anayefanana naye kwa sura.

Lakini, hata kama ni picha yake ya kweli au ya kuchongwa, chombo kilichotumika kumdhihaki kimekuwa kinawadhihaki wananchi wengine wengi tu; raia wema wasio mali ya jamii, na ambao wana haki ya usiri na faragha kama yeye, labda hata kuliko rais mwenyewe.

Hawa wanaochorwa kila siku wana utu na ubinadamu wenye kasoro kuliko wa kiongozi wetu? Yaani wengine si binadamu, hawana haki ya faragha, isipokuwa kiongozi wetu? Huo si ubaguzi?

Au ngoja tuliweke hivi. Kama uongozi ni taasisi na taswira ya taifa, si ndilo taifa hilo hilo lenye watu hao hao wanaoanikwa kila kukicha kwenye mitandao hiyo hiyo?

La msingi hapa, tukubaliane. Ama tusimdhihaki mtu yeyote kabisa, tuvizuie vyombo hivyo kufanya dhihaka hiyo (jambo ambalo halikubaliki); au tuviache viwadhihaki wote ambao wanauzika na wana mvuto kwa wasomaji wa mitandao hiyo.

Najua dhihaka nyingine hazipendezi, lakini ni sehemu ya kazi za vyombo vya habari. Na kwa utamaduni uliorithiwa kwa miaka mingi duniani, dhihaka tamu ni zile zinazoelekezwa kwa wakubwa, si kwa watu wadogo wadogo wa kawaida.

Wasiopenda kudhihakiwa wasiutafute ukubwa. Ukubwa ni ubabu. Na haki mojawapo ya babu ni kudhihakiwa na kutaniwa. Na utani mzuri ni ule usiopendeza; ule unaouma, uwe wa kweli au wa uongo; ule unaodhalilisha!

Lengo la dhihaka ni utani tu wenye nia ya kulegeza hisia na mishipa ya fahamu, kuburudisha na kuchangamsha nafsi.

Watu wajinga, wababe na katili ndio watapoteza muda wao kukimbizana na wajukuu wanaomdhihaki babu yao.

Wenye akili timamu watakaa chini kuungana na umma wa raia wengine wanaocheka hadi machozi yanawatoka.

Hata babu mwenyewe hapaswi kukasirika anapotaniwa. Ndiyo ukubwa; ndiyo ubabu. Na kwa wanaojua, isipokuwa kwa wahafidhina tu, haya ni matumizi mazuri ya vyombo vya habari.

Hakuna haja ya serikali kutumia mabavu kuwaandama wajukuu, na hatimaye kugundua kuwa yule aliyechorwa anafanyiwa kitendo kiovu, si kiongozi wetu, bali ni picha ya mtu anayefanana naye. Makali ya mjadala yatakuwa yameisha.

Lakini mjadala wa pili uliokuwa mkali ni ule uliotokana na tuhuma za Mengi dhidi ya baadhi ya wafanyabiashara wazito wanaohusishwa na ufisadi uliokubuhu. Mengi naye ametugawa katika makundi.

Katika kumpongeza au kumlaumu, baadhi ya wananchi wanasema amelipuka. Wengine wanasema amefyatuka. Wengine wanasema ameropoka.

Wapo pia wanaohoji: “Mengi amepata wapi ujasiri huu? Ametumwa na nani? Mbona ametaja wanaojulikana na wengine tayari wako mahakamani?

Mbona ametaja wenye rangi zinazofanana fanana tu? Mbona ameacha kuwataja hao wengine tunaowahisi? Ana masilahi gani katika hili? Ni siasa au biashara? Ni ushujaa au unafiki? Ni usamaria mwema au unabii? Ni sifa binafsi au masilahi ya taifa?”

Yameulizwa mengi na yataendelea kujadiliwa. Lakini ukiyatazama kwa kina, maswali mengi yanayotilia shaka hatua na kauli hii ya Mengi yanamtazama yeye msemaji, hayajadili alichosema.

Bahati mbaya, hata baadhi ya watuhumiwa walipohojiwa na vyombo vya habari, nao hawakujadili tuhuma zilizotolewa dhidi yao. Walijadili u-mengi wa Mengi, matatizo yake ya kifamilia na hisia zake binafsi.

Na wengine wakahitimisha kwamba kuwaita waandishi na kuwaeleza hayo (yasiyo mapya) na kuyatangaza kwa kipindi maalumu katika televisheni anayomiliki, ni matumizi mabaya ya vyombo vya habari.

Hebu tujiulize. Vyombo vya habari havipaswi kutumiwa na wanaovimiliki? Jambo alilojadili Mengi halina masilahi ya kitaifa? Mtu asiyekuwa na masilahi ya kisiasa hawezi kupambana na wanasiasa mafisadi? Masilahi yake ya kibiashara yanamzuia kupinga kile ambacho sote tunakipinga?

Kama aliyosema yangesemwa na mtu mwingine, yangekuwa na ukweli kuliko aliousema yeye?

Kwa wasifu wake katika jamii, na kwa kupambana na watu wenye wasifu kama wa kwake kibiashara, hata kama walikwaruzana mahali fulani kimasilahi, Mengi hajaongeza nguvu ya wapambanaji wanyonge katika vita dhidi ya ufisadi?

Ni kweli kwamba vita dhidi ya mafisadi wakubwa kama hawa inaweza kupiganwa na kufanikiwa bila nguvu ya watu wakubwa na wazito kama Mengi? Makosa na kasoro binafsi au za kibiashara ya Mengi yanaondoa ukweli wa kile alichojadili?

Na vyombo vya habari visipotumika kupigana na ufisadi kama huu, ni matumizi gani mazuri yanayozungumzwa na yanayotarajiwa?

Kwa nini tunaviamini vyombo vya Mengi vinapotumika wakati wa kampeni kuwafagilia watawala, lakini hatutaki kuviamini wakati huu vinapowagusa na kuwatikisa kidogo?

Hata kama kuna lolote nyuma ya pazia, Mengi anastahili lawama au pongezi? Kwa wanaoujua mwenendo na ukuaji wa mfumo wa vyombo vya habari nchini, mchango wa Mengi katika kukuza uhuru wa habari unaweza kupuuzwa? Yeye anayeshiriki kukuza uhuru huu hana haki ya kutumia vyombo hivyo?

Swali la ziada. Tunatafuta watu wasio na masilahi yoyote kabisa ndio wapambane na ufisadi huu? Wapo? Wataweza? Ni nani kati yetu anayeweza kujitangaza akaaminika kwamba hana masilahi yoyote ya kisiasa, kibiashara au kijamii katika masuala haya tunayojadili?

Nimejiuliza maswali hayo yote na kuhitimisha kwamba, Mengi anastahili pongezi, si lawama.

Ukiwasikiliza hata wanaotaka tumzomee kwa hili, utagundua kwamba nao wana masilahi wanayolinda kikazi, kibiashara au kijamii yanayomhusisha Mengi. Au wengine hawajaitafakari hoja yake kwa sababu ya hisia; wamemtazama yeye.

Kila mtu ana masilahi anayotetea, lakini katika hili Mengi amejiunga na wengi wanaotetea masilahi ya taifa.

Na wale ambao wamekuwa wakimtuhumu kwa kuwasaidia sana watawala kupitia vyombo vyake, wanafurahi kwamba walau sasa Mengi ametangaza ‘kuongoka.’

Si kwamba amekamilika. Zipo kasoro, na yapo mambo kama mawili yanayomponza. Kwanza, ushirika wake wa kikazi na watawala ndiyo umemgonganisha na baadhi ya wapambe wa watawala.

Hata hao anaowatuhumu wanadaiwa kufanikiwa kifisadi kutokana na ukaribu wao na mifumo ya utawala.

Kwa sababu hiyo, anawatuhumu akijua kwamba nao wanamfahamu, na sasa wanaandaa mashambulizi mazito dhidi yake kama walivyomfanya Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe.

Lakini, hata wakimshambulia, hoja inabaki pale pale. Kuna ufisadi au hakuna? Wanahusika au hawahusiki? Tuwasifu au tuwabane? Hapa ndipo mjadala wenyewe unapopaswa kujikita.

Wao wana masilahi; naye ana masilahi. Nasi tuna masilahi. Lakini kwa suala hili, baadhi yetu tunafurahi kwamba Mengi amejitokeza hadharani kwa kishindo.

Wasifu wake ni silaha kubwa na nyeti. Ni nguvu ya nyongeza katika mapambano haya. Ni mtu anayejua mambo ya ndani. Ni vigumu kumpuuza.

Katika hili, kauli yake ni kubwa, nzito na makini; na inaaminika kuliko ya mkulima, mfugaji, mvuvi au mchuuzi mdogo mdogo asiyejua mwenendo wa mifumo ya kibiashara na kisiasa ilivyosukwa kwenye ufisadi wa watawala.

Itakapoletwa mada ya kujadili kasoro za Mengi, wanaozijua wajitokeze wazijadili; lakini si katika hoja hii ya sasa. Haiwezekani wote wakamuunga mkono, lakini si vema kuwaruhusu watu wapotoshe hoja kwa kumtazama msemaji badala ya kujadili alichosema.

Jambo la pili linalomponza Mengi katika hoja hii ni madai yake kwamba anamsaidia rais kupambana na ufisadi. Je, inawezekana msaada huu huu anaompa rais ndiyo umemzuia kuwataja hao mapapa wengine aliowaweka kiporo?

Analinda nini? Kwa nini amewatanguliza hawa watano? Mjadala huu hauwezi kukamilika bila majibu ya maswali haya kupatikana.

Na hoja yake inaingia kasoro pale anaposema kwamba mafisadi papa hawakamatiki? Maana yake nini? Nani anashindwa kuwakamata? Hii si tuhuma ya ziada kwa rais ambaye ndiye mkuu wa majeshi yote na TAKUKURU?

Na kama rais anashindwa kuwakamata si kweli kwamba anawalinda? Sasa iweje Mengi anasema wanaopiga vita ufisadi wanamsaidia rais?

Au ndiyo mbinu ya kula na kipofu, anaogopa kumshika mkono?

Yeye yuko karibu na rais kama walivyo hao aliowatuhumu. Tofauti yao ni viwango vya ukaribu. Wanaoelewa mambo yalivyo wanasema kwamba watuhumiwa wa Mengi wako karibu zaidi na Ikulu kuliko yeye.

Baadhi yao ni waasisi wa jitihada zilizomfikisha Kikwete hapo alipo. Wengine wamekuwa washauri wake wasio rasmi katika siasa na uchumi.

Kwa jinsi hii ndivyo rais alivyohusishwa (bila kutajwa wazi wazi) katika kashfa ya Richmond tangu awali. Walimshauri, walimshirikisha; na aliwaamini.

Baadhi yao wamekuwa na nguvu kubwa Ikulu kuliko hata mawaziri katika maamuzi kadhaa makubwa kitaifa.

Baadhi ya watuhumiwa wa Mengi ndio wamefaidika sana na miradi na tenda kubwa kubwa za serikali hii kabla mambo hayajaanza kuwageuka.

Niliwahi kuandika hapa kwamba mmoja wa watuhumiwa wa Mengi aliupatia mtandao pesa nyingi wakati wa kampeni, kiasi kwamba baadaye washauri wa rais walipomwambia asimshirikishe masuala ya serikali (kwa sababu walitilia shaka dili zake), rais aling’aka kwamba si utu kumtenga kabisa kwa sababu aliwasaidia sana.

Mwingine ni yule aliyewahi kutuhumiwa ‘kuuweka mfukoni’ uongozi wa Mkoa wa Iringa wakati akitafuta kumilikishwa mradi wa makaa ya mawe ya Mchuchuma na Liganga.

Aliwaweka vizuri madiwani, mbunge wa eneo husika, mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa ili wamsaidie kupata mradi kirahisi. Kuna siku tuliwahi kumbamba mkuu wa mkoa akiingia kwenye hoteli ya ‘mwekezaji’ huyo jijini Dar es Salaam, na kujisajili kitabuni kwa jina lisilo lake.

Ndiye mwekezaji huyo aliyekuwa anatamba kwamba alisoma na kucheza na mzee, na kwamba mchango aliotoa kwenye kampeni ndiyo gia ya kumrahisishia kupata mradi wa Mchuchuma. Yapo mengi. Waliyasema wazi wakati wa neema, sasa mambo yamebadilika, kauli zao zinawarudi.

Hatuwezi kumbeza Mengi anayepambana na watu wa aina hii. Lakini pia hatuwezi kukubaliana naye kwamba anamsaidia rais. Ningekubaliana na Mengi kama angesema kwamba anawasaidia wananchi wanyonge, walipa kodi, wanaonyonywa na mafisadi.

Kama rais angedhamiria, hao jamaa wasingekuwa na jeuri tena. Wasingepewa muda na fursa ya kurekebisha mambo yao Kwa mamlaka aliyonayo, rais anaweza kuwashughulikia hata watuhumiwa waliotumia majina bandia kufanya uhalifu.

Haiwezekani kwamba yeye hajui, lakini maelfu ya wananchi wanajua yaliyotokea na jinsi yalivyotokea. Hatujaona jitihada za kimfumo za kukomesha ufisadi huu.

Kwa hiyo, tukubaliane kimsingi kuwa Mengi amefanya jambo jema; kwamba naye ana kasoro lakini hazifuniki hoja yake; kwamba alipowataja hawa hakutazama rangi au nasaba zao bali matendo yako; na kwamba alipaswa kuwataja wote.

Tunaweza kumpa haki ya kuhifadhi baadhi ya majina kwa wakati huu, kwa hekima na sababu anazojua.

Tukubaliane pia kwamba kumiliki vyombo vya habari hakumnyang'anyi Mengi uraia wala haki ya kuvitumia. La msingi avitumie kusema ukweli kama raia mwingine yeyote.

Tukubaliane pia kwamba Mengi hajaropoka, bali amelipuka na kulipua bomu; na kwamba inawezekana hakutumwa na mtu (nani? Rais?) bali dhamiri yake, kwa sababu anazojua.

Tusipuuze pia ukweli kuwa maisha yamejaa mashindano. Kila mtu anashindana na watu au masuala yanayozunguka maisha yake au na wengine wenye masilahi kama yake, lakini mashindano hayazuii ukweli kuchomoza.

Mashindano hayana ubaya kama yanatusaidia kuibua yale ambayo bila ugomvi yasingeibuka, na hata kama yangeibuka, wadogo wangeogopa kuyagusa.

Kwa maoni yangu, kama tungekuwa na kina Mengi wengine kama watano, nchi hii ingerekebishika kirahisi, na jeuri ya wakubwa na wapambe wao ingekoma.

Kwa hali ya sasa maskini hohe hahe hawawezi kupambana na kushinda mafisadi papa hawa wanaolindwa na pesa chafu na mamlaka za dola. Biashara zao zimeshikamana na siasa za chama tawala (CCM); na hata wakiwa kimya, wanakuwa na kauli nzito na ushawishi mkubwa kwa watawala.

Ndiyo maana baadhi yetu tunafikiri kwamba, ingawa Mengi anadai kwamba anamsaidia Rais Kikwete katika hili, inawezekana anapambana naye bila kujua.



juu