NILIMALIZIA makala ya Jumapili iliyopita kwa kuhoji kama mfanyabiashara maarufu Reginald Mengi alikuwa anamsaidia Rais Jakaya Kikwete au alikuwa anapambana naye.
Wiki hii Profesa Ibrahim Lipumba amehitimisha kwa kusema Mengi anajikomba kwa Kikwete.
Mimi na Lipumba tunakubaliana kwamba ufisadi unalelewa na mfumo wa utawala; na si sahihi kabisa kudanganya Watanzania kuwa rais anapinga ufisadi wakati mafisadi wamo kwenye ‘kwapa’ la serikali yake, na ndiyo injini inayoendesha siasa za chama tawala.
Wengine walioungana nasi ni vijana wa CCM kutoka Tabora waliojitokeza kumteteta Mbunge wao wa Igunga, Rostam Azizi, ambaye alitajwa na Mengi kuwa miongoni mwa mafisadi papa.
Walisema Mengi amekuwa anapambana na wasaidizi wa rais. Hivyo, si kweli kwamba anamsaidia rais kwa sababu anahoji uwezo wake na kutilia shaka uteuzi wake.
Kwa hiyo, Mengi anampaka rais mafuta kwa mgongo wa chupa. Bila kudhamiria, vijana hawa walituunga mkono sisi tunaoamini kwamba huwezi kupambana na ufisadi nchini halafu ukawa kipenzi cha rais au serikali.
Ndiyo sababu baadhi yetu tunatazamwa kwa jicho la ‘kihaini’ kwa kuwa tunataka kung’oa nguzo iliyoisimika serikali inayongozwa na watu wa aina ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sofia Simba, ambao wanajizungusha kwenye hoja za Mengi ‘kuingilia mahakama’ wakati wakijua kuwa alichojadili Mengi si kesi iliyo mahakamani, na waliotajwa na Mengi si wote wako mahakamani.
Hivyo hatushangai kauli ya serikali kumchunguza Mengi kuhusu matumizi ya vyombo vya habari, kwa sababu tunajua ilivyo tayari kumng’ata yeyote anayeishika ‘sehemu za siri.’
Badala ya kujadili hoja yake na kuchunguza tuhuma alizotoa, au badala ya vyombo vya sheria kumtaka avipe ushahidi wa nyongeza wa madai yake, wanamwandama na kumtisha.
Kibaya zaidi, serikali (na watu wake) inataka kutuingiza kwenye mtego wa kutazama rangi ya ngozi ya wale waliotuhumiwa ili kujenga hoja mpya na dhaifu kwamba Mengi anachochea ubaguzi wa rangi. Wanamwekea mdomoni maneno na hisia ambazo hazikuwa kwenye ajenda asilia.
Maana yake ni kwamba wameshadhamiria kuwa baadhi ya watu, hata wakiwa na tuhuma za kweli, wasiguswe kwa sababu itaonekana ni ubaguzi wa rangi!
Maana ya ziada ni kwamba, kwa kuwa walishaamua kuwatetea, kama wangetajwa wengine, kingetumika kigezo cha kuangalia wengi wanatoka kabila gani au ni wafuasi wa dini gani – mambo ambayo hayana nafasi katika mjadala wa ufisadi.
Wanataka kuleta hisia kwamba Mtanzania mwenye asili ya Kiasia, kwa mfano, akimtuhumu Mtanzania mzawa mweusi atakuwa amembagua kwa rangi yake!
Huu ni upuuzi! Na inasikitisha kwamba unaendekezwa na wale wanaosimamia utawala wa nchi, na wananchi wengine wasiopembua kwa kina dhana ya ubaguzi wa rangi au wasio na msimamo au wanaoyumbishwa kirahisi.
Ubaguzi wa aina yoyote ile haufai kushabikiwa na mtu mwenye akili timamu. Kila mtu ana imani, nasaba, kabila, rangi ya ngozi, kiwango cha elimu, uwezo wa kiuchumi na kadhalika. Lakini mambo haya yasitumike kama kigezo cha kuwabagua wengine, kufunika hoja za msingi, au kuwakingia kifua wanapotuhumiwa au kubeza hoja zao wanapojitetea.
Wala tusipotoshe maana ya kile alichofanya Mengi. Tuhuma za Mengi dhidi ya wafanyabiashara wenzake, zina tofauti gani na tuhuma za Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro, dhidi ya ufisadi katika umiliki wa mgodi wa Kiwira na mingineyo? Tuache hoja ya Kimaro tujadili rangi ya ngozi ya watuhumiwa wake au makabila yao au masilahi ya kisiasa ya Kimaro?
Zina tofauti gani na nyingi zilizotolewa na wapambanaji kama Dk. Wilibrod Slaa, Anne Kilango, Zitto Kabwe, Hamad Rashid Mohammed na wengine?
Hii ndiyo mbinu mpya ya serikali kuwasaidia mafisadi kwa kutafuta jinsi ya kuwashambulia wanaotoa tuhuma? Raia wakizuiwa kutoa tuhuma wafanye nini?
Na hao waliosombwa na mbinu hii ya serikali, wanaotaka kumnyamazisha Mengi, wanafikiri kwamba wakiisaidia serikali kumnyamazisha, wao watapata mahali pa kusemea? Au wanadhani wao wataendelea kuishi kwa fadhila za serikali na wapambe wake hadi lini?
Hivi miaka 48 baada ya uhuru, bado wapo Watanzania ambao wanadhani rangi ya ngozi ya mtu ni suala la msingi au kinga ya kutosha anapojikuta matatani?
Taifa hili bado lina watu wanyonge kiasi cha kudharauliana na kubaguana kwa misingi ya rangi ya ngozi? Ni haki tuwaruhusu viongozi wa serikali wapandikize hoja hizi mahali zisipohusika ili kufunika udhaifu wao?
Inasikitisha kwamba baadhi ya wapambanaji dhidi ya ufisadi wamebaki kujenga hoja za kinadharia kuhusu usawa na haki, lakini wanashindwa kuona kwamba mnyanyasaji mkuu na mvunjaji mkuu wa haki za wanyonge anatumia hoja zao kudumisha utumwa wa kifikra na kuua mapambano.
Kwa kiasi fulani, serikali imefanikiwa kuwachanganya wananchi na kuwafanya wajadili suala tofauti na hoja ya msingi; jambo ambalo limewahakikishia mafisadi ulinzi wa serikali katika mazingira yasiyotarajiwa.
Kwa mara ya kwanza ndani ya miaka miwili ufisadi umepata rutuba ya kuusitawisha kwa kuwa wapambanaji wameanza kupoteza lengo, kuchoka mapambano, na kuanza kupigana vikumbo wao kwa wao.
Tazama mfano huu: Joka kubwa linaingia nyumbani kwako. Una silaha hafifu. Ndani kuna watoto wachanga wasioweza kukimbia. Unapiga kelele majirani wanakusanyika wakiwa na silaha mbalimbali.
Miongoni mwao unamuona mgomvi wako wa siku nyingi, akiwa na bunduki yenye risasi za moto, na akiwa na nia ya kuliua joka. Lakini hutaki kumruhusu aingie nyumbani mwako, wala hutaki kutumia bunduki yake kuua joka hilo.
Badala ya kulifuata joka ndani ya nyumba mnaanza kubishana na majirani kuhusu uhalali wa kumruhusu mwenye bunduki kuliua joka.
Hata kama hatimaye mtamaliza ugomvi na kuamua kuchukua hatua, watoto hao ndani ya nyumba watanusurika?
Ndivyo ninavyoutazama pia mjadala wa Mengi na ‘mapapa wa ufisadi.’ Sijaona mtu aliyekuja na hoja za kuridhisha kutetea waliotuhumiwa na kuthibitisha usafi wao.
Wengine wamejaribu kumkosoa Mengi, wakateleza na kuisaidia serikali na mafisadi.
Mfano mzuri ni Profesa Lipumba. Aliposema Mengi anajikomba kwa Kikwete alikuwa na hoja. Lakini alipotoka katika suala la rangi za ngozi za watuhumiwa na hoja kwamba Mengi alipaswa kupeleka madai yake mahakamani.
Maana Mengi anataka tuanze kupambana na ufisadi kwa kuwabana wale aliowaita mapapa wa ufisadi.
Lipumba anataka tuanze kwa kudhibiti mfumo wa utawala, na watawala wenyewe wanaowalea mafisadi.
Nani yuko sahihi? Kwa hoja ya Mengi, ufisadi wa watawala unakuzwa na wafadhili wao. Wanasiasa wengi ni watu wa kawaida, lakini wanapata madaraka na jeuri inayoambatana nayo kutokana na ufadhili wa wafanyabiashara hawa tunaowatilia shaka.
Kwa hiyo, kama wafadhili watadhibitiwa, wanasiasa watanyong’onyea kwa kiasi kikubwa. Rushwa kwenye uchaguzi itapungua. Fadhila za kurejesha kwao kutoka serikalini zitapungua au zitakoma.
Jeuri ya pesa chafu za wanasiasa itakwisha. Ulinzi wa serikali kwa mafisadi utapungua au utakoma. Vita dhidi ya mafisadi itapata mwelekeo mpya.
Mengi ameanzia kule aliko – kwenye biashara – na analeta mbinu inayofanana na mazingira yake ya kikazi. Yuko sahihi.
Lipumba anaamini kwamba wafanyabiashara wasingefurukuta kama watawala wangekuwa makini. Kama tungekuwa na mfumo unaosimamiwa na watu wenye dhamira safi, vita ya ufisadi ingekuwa nyepesi.
Watawala wana nyenzo zote muhimu katika vita hii. Wana nguvu ya kitaasisi, kisheria, kimadaraka na hata kifedha. Wasichokuwa nacho ni dhamira ya kweli ya kupambana na ufisadi.
Kwa hiyo, kama tunataka kupambana na ufisadi, tuanze kwa kuwabana wao. Ndiyo maana anasema kwamba yeyote anayetaka kuwabana mafisadi hana sababu ya kujipendekeza kwa serikali, maana hiyo ndiyo inapaswa ibanwe.
Lipumba pia anaanzia kule aliko. Anatupatia mbinu inayotokana na mazingira yake kikazi. Yeye ni mwanasiasa, anataka tuanze na wanasiasa. Ana hoja.
Ni kweli, tukiwabana watawala, ufisadi utapungua kwa maana nao watawabana wapambe wao wanaowaingiza katika matata.
Lakini njia za kuwabana watawala zipo nyingi. Hata hii ya kuwabana wapambe wao, inaweza kutusaidia kuwafikia watawala, maana wao hawafikiki.
Ikumbukwe kuwa kwa sehemu kubwa, jeuri ya watawala inatokana na nguvu kubwa ya misaada ya hali na mali ya kifisadi. Bila misaada hii, baadhi yao wasingekuwa hapo walipo.
Ndiyo maana serikali imekuwa ikihaha kuwatetea. Alianza Kingunge Ngombale-Mwiru Septemba 2007 kuwatetea mafisadi baada ya bomu la Mwembe Yanga.
Wakafuatia wastaafu kadhaa na mawaziri wakasambazwa nchi nzima kuzima moto wa wapinzani; akahitimisha Rais Jakaya Kikwete katika mkutano wa hadhara mjini Arusha kwamba wapinzani wanajifanya walalamikaji, polisi, mahakimu na askari magereza.
Alisema kauli zao ni kelele za mlango hazimnyimi usingizi. Hatujasahau.
Leo atapata wapi haki ya kujidai na hata kusifiwa kuwa anapambana na ufisadi?
Watu wale wale walio katika orodha ya mafisadi wanajitapa kwamba wanapambana na ufisadi, na sisi tunakubali? Wanamdanganya nani? Ni lini wametambua kwamba nchi hii inakabiliwa na ufisadi?
Ni bahati mbaya kwamba baadhi ya washambuliaji wa Mengi wanaazima maneno yale yale ya Kikwete aliyoyatolea Arusha miaka miwili iliyopita.
Nilipomsoma Absalom Kibanda katika mfululizo wa makala zake: “Ni vita ya ufisadi au urais?” nilihoji mwelekeo wa hoja yake na nilihitimisha kwa kumjibu kimya kimya kwamba ni zaidi ya urais. Ni masilahi.
Hata wanaotetea na kuunga mkono hoja ya Mengi wana masilahi kadhaa wanayotetea; ya kwao au ya wengine au ya jamii.
Nimewasikia wadau wengine waliozungumzia sakata hili. Hoja za waliotofautiana na Mengi hazikuwa na nguvu ya kutosha kumnyamazisha. Wengi wao wameacha kujadili hoja yake, wakajikita katika kujadili usafi na uchafu wa Mengi.
Lakini kama usafi wa msemaji ni kigezo, hata wao wenyewe wasingethubutu kuandika hayo wanayoandika au kutamka hayo waliyotamka.
Maana kama wao wasio safi wanadhani wanaweza kuandika au kusema ukweli dhidi ya Mengi, basi na Mengi aliye mchafu anaweza kusema ukweli juu ya wengine. Kwa mantiki hiyo basi, ama tujadili walichosema wao dhidi ya Mengi au kile alichosema Mengi dhidi ya wale aliowatuhumu.
Niliwahi kusema huko nyuma kwamba tabia hii ya kuacha hoja na kumwandama mtoa hoja ni mojawapo ya magonjwa ya kiakili yanayomnyima binadamu fursa ya kufuata misingi ya mantiki katika kujadili suala lililo mbele yake.
Katika falsafa, upotofu huu wa kuacha hoja na kumshambulia mtoa hoja unajulikana kwa jina la Kilatini: ad hominem argumentum. Ni ugonjwa ambao lazima tuutibu.
Lakini njia ya kuua hoja ya Mengi ni moja na rahisi. Wajitokeze watu wachambue na kufafanua usafi wa waliotuhumiwa katika yale waliotuhumiwa au watuhumiwa wenyewe waende mahakamani ushahidi ukusanywe, mwenye hatia ajulikane.
Ndiyo maana nakubaliana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwamba wale wanaodhani kwamba wamekashifiwa na Mengi wachukue hatua za kisheria.
Jambo tunalojiuliza ni je, wale wale walioogopa kumshitaki Dk. Slaa kwa kuwatuhumu, wana ujasiri wa kweli kumshitaki Mengi?
Lakini kuziba hoja ya Mengi kwa visingizio vya makabila na rangi za watuhumiwa, ni utoto katika mjadala wa watu wazima.
Ni makosa makubwa kuficha ufisadi nyuma ya dini, makabila au rangi za ngozi za watu.
Ni bahati mbaya kwamba baadhi ya wapambanaji wamenaswa na ulimbo wa serikali, wakaingia kwenye mkumbo bila kujua.
Baada ya watu kuanza kukoroga hoja ya Mengi, mafisadi wanaamini tumepoteza lengo; maana wanaona baadhi ya wapambanaji wameanza kuelemewa na silaha, wanaziweka chini kwa kisingizio kwamba ‘hawana upande’ katika suala hili ili waonekane wanatenda haki kwa pande zote.
Wanasahau kwamba mafisadi wenyewe hawafuati haki, bali masilahi; na wamevuruga misingi ya haki ili wanaoifuata misingi hiyo waikose haki lakini waridhike na watakachokipata.
Tukubaliane kwamba kazi ya kizazi hiki si kutetea uozo wa kizazi kinachopita; na kwamba sehemu ya wajibu wetu ni kuondoa kutu katika akili na fikra butu za wanajamii wenzetu.
Hatuwezi kusubiri kizazi hiki kife ndipo tuanze kuwakomboa Watanzania kifikra. Tutaanza na kizazi hiki hiki kilichokorogwa mawazo kwa kukaririshwa mambo; kizazi cha watiifu na waoga wa mamlaka dhalimu, kizazi cha wanaoridhika na majibu mepesi na kauli rasmi kwa vile tu zimetolewa na wakubwa.
Tukisubiri kizazi hiki kiondoke, na sisi wenyewe hatutakuwapo. Lakini ili tukikomboe kizazi hiki kilichokorogwa mawazo, lazima na sisi tukikoroge pia; ndipo tuanze pole pole kukisafisha.
Tutampuuza Simba na wenzake maana wanataka kutugawa ili tuache hoja, tuanze kupambana wenyewe kwa wenyewe, wao wapite katikati yetu.
Ninachoamini kwa sasa ni kwamba dhihaka dhidi ya Mengi ni suala la wakati tu; zitapita. Kipimo alichopimiwa Dk. Slaa baada ya Mwembe Yanga ndicho hicho atakachopimiwa Mengi.