LEO nitajadili maudhi mawili kutoka serikalini - wizi wa vigogo kwa mgongo wa jeshi, na ukubwa wa matumbo ya mawaziri.
Tumeingia katika zama za siasa za matumbo ya vigogo, ambayo wao wanadhani ni makubwa kuliko ya wananchi zaidi ya milioni 40 nchi nzima.
Na sasa wamekuja na mpya; kwamba matumbo yao yalindwe kwa kodi zetu na vyombo vyetu vya dola, eti kwa sababu ndani ya matumbo hayo ndimo ulimo usalama wa taifa letu!
Njaa, shibe, tamaa na wizi wa vigogo vimepewa kinga ya usalama wa taifa. Na sasa, kwa makusudi au kwa kutokujua, wameamua kulichafua jeshi letu kwa kulifanya uchochoro wa wizi.
Ni wazi, viongozi wa mataifa mengi hupenda kujificha nyuma ya majeshi wanapokuwa wanafanya mambo ya kifisadi wasiyotaka yahojiwe na umma.
Lakini, kwa Tanzania, jambo hili si neema, na halikubaliki kwa sababu ni kudhalilisha wanajeshi wetu waadilifu na wananchi wetu waaminifu. Ni kejeli kwa wananchi wapiga kura na walipa kodi wa Tanzania.
Na hili ni jambo ambalo lisingepaswa kuhusishwa na utawala wa watu waliojiita kizazi cha ari, nguvu na kasi mpya. Lakini hizi ndizo rangi zao halisi ambazo kwa miaka mitatu na nusu sasa zimeshamiri na kuwaumbua.
Ni utawala ulioanza kazi kwa matanuzi hotelini Ngurdoto, Arusha, kupeana semina elekezi; utawala ulioshindwa kazi ya msingi, lakini uko tayari kujipongeza kwa matanuzi ya ziada, na kujitengea sh bilioni 30 za ‘chai ya vigogo’ na takrima ya wageni wao katika bajeti ya serikali.
Na kama matokeo ya semina elekezi za Ngurdoto na ziara za wakubwa wizarani ndiyo haya tunayoshuhudia leo serikalini na bungeni, wananchi wote tuna haki ya kuungana na Mbunge Lucas Selelii aliyewalaani mawaziri wote na wakubwa wao!
Hatuwezi kuendekeza utawala unaokula njama za makusudi kuiangamiza nchi yetu, wala hatutakubali dhana hii inayojengeka serikalini kivitendo, na kulindwa kisheria, kama tulivyoshuhudia kwenye bajeti ya mwaka huu, kwamba matumbo ya watu wapatao 40 tu yapewe heshima, thamani na haki kubwa kuliko ya matumbo ya Watanzania wote!
Maana yake nini? Kwamba vigogo peke yao wanajitengea bajeti ya chai ya sh bilioni 20, na takrima ya wageni wao ya sh bilioni 10, na Bunge letu linatumika kujadili na kupitisha kashfa hiyo, katika wakati huu mgumu tuliomo kiuchumi, huku wizara kubwa zinazohudumia wananchi zaidi ya milioni 40 zikitengewa mafungu madogo ya pesa, ni ishara ya wazi kwamba kasi ya wenzetu hawa inatupeleka pabaya.
Tazama, Ikulu imetengewa sh bilioni 7.3; Ofisi ya Waziri Mkuu imetengewa sh bilioni 5.4; Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imetengewa sh bilioni 12; Mahakama Kuu imetengewa sh bilioni 17.8; Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma imetengewa sh bilioni 17.4; Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo imetengewa sh bilioni 15.8.
Wizara ya Katiba na Sheria imetengewa sh bilioni 6.8; Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetengewa sh bilioni 11.7; Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki imetengewa sh bilioni 13.9; Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Vijana imetengewa sh bilioni 9. Zipo wizara nyingine zilizotengewa kiasi kidogo kuliko bajeti ya chai ya vigogo.
Haya ndiyo yanayoshangiliwa na ndugu zangu wapambe wa CCM wanaoipongeza serikali kwa kutekeleza ilani ya chama chao kwa asilimia 100! Nadhani hapa kuna tatizo jingine la kujua maana halisi ya asilimia 100.
Hawatafakari kwa nini idadi ya maskini inaongezeka, kwa nini elimu yetu inadidimia, kwa nini afya yetu inatetereka, na kwa nini taifa kijumla linazidi kuwa maskini wakati tuna rasilimali nyingi kiasi cha kutenga chai ya vigogo na takrima ya wageni kwa bilioni 30!
Nchi inateketea, watawala wananeemeka! Hii ndiyo ilani inayotekelezwa. Na hii inanikumbusha kauli ya mwana CCM mmoja miaka minne iliyopita, katika maandalizi ya kampeni za uchaguzi mkuu wa 2005.
Nilikutana na mpambe huyo wa mgombea urais wa CCM, mjini Dodoma, akanitania akisema: ‘Mbona unatupiga vita hata kabla hatujala?’
Baada ya uchaguzi, mpambe huyu aliteuliwa kuwa naibu waziri. Akaingia kwenye kundi la walaji, na baadaye akapanda cheo. Sasa ni waziri mwandamizi na mmoja wa wapambe wakuu wa rais.
Kula ndiyo dhana iliyokuwa (na iliyomo) vichwani mwao. Miaka minne iliyopita imetudhihirishia hili na kutuonyesha watawala wetu wakipambana na wananchi ili kulinda na kuendeleza ufisadi waliourithi, walioutumia kufika pale, na wanaoujengea misingi mipya ili waendelee kuneemeka, huku wakisahau adha za wananchi wao.
Hilo ndilo alilokuwa anajadili Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, wiki hii alipowakejeli bungeni watani wake wa CCM wanaojipongeza kwa asilimia 100 za ufanisi wa ilani yao, huku taifa likiteketea.
Alisema hivi: ‘Wakati Serikali ya Awamu ya Nne inachukua madaraka, asilimia 11 ya watoto waliokuwa wanazaliwa walikuwa wanakufa kabla hawajatimiza umri wa miaka mitano. Leo ninavyozungumza nanyi, kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi, katika kila watoto 1,000 wanaozaliwa Tanzania, watoto 134 wanafariki kabla hawajatimiza umri wa miaka mitano. Tunapoteza watoto 800,000 kila mwaka; Mkoa wa Lindi una idadi ya watu 800,000.
‘Katika kila wanawake 100,000 wanaopata ujauzito Tanzania, wanawake 578 wanafariki dunia kwa matatizo ya uzazi. Takwimu hizi zinaonyesha kila saa inayopita katika nchi yetu kuna mwanamke mmoja anafariki kwa sababu ya matatizo ya uzazi.
‘Asilimia 44 ya Watanzania ni watoto walio chini ya umri wa miaka 15. Nusu ya Watanzania wako chini ya umri wa miaka 17; Lakini takwimu za serikali zinaonyesha kwamba asilimia 38 ya hao watoto wamedumaa…masuala ya lishe. Katika kila watoto 10 wa Tanzania, watoto wanne wamedumaa. Tunajenga taifa la namna gani?’
Hoja ya Kabwe ina sehemu mbili. Kwanza, haya si mazingira ya watawala kupongezana na kujitengea sh bilioni 30 za chai na takrima. Pili, anataka kujua, hiyo ilani wanayojisifia kuitekeleza kwa asilimia 100 ni ilani gani, kwa faida ya nani? na hizo asilimia zinaonekana kwa vigezo gani?
Je, ilani hii ndiyo inawaagiza watawala kutumia mgongo wa jeshi letu kutetea wizi wa kimfumo, kwa kutumia Bunge letu na kutuzuia kuhoji ufisadi wao katika Kampuni ya Meremeta inayotuhumiwa kukwapua sh bilioni 155, za walipa kodi, ambazo ni nyingi kuliko hata za ufisadi wa EPA?
Ilani hii ndiyo imemshika mikono Rais Jakaya Kikwete (kinara wa kasi mpya) asitekeleze mapendekezo ya ripoti ya Kamati ya Bomani kuhusu tuhuma ya ufisadi katika kampuni za Meremeta, Tangold, na Tanpower Resources Ltd, kwa zaidi ya nusu mwaka sasa?
Ilani yao ndiyo ilimtuma Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ajiapize kwamba liwalo na liwe, hatajadili suala la Meremeta bungeni kwa sababu linahusu usalama wa taifa?
Lakini swali la msingi katika hoja hii ya Meremeta ni hili: Ni lini wizi wa rasilimali zetu umekuwa sehemu ya usalama wa taifa?
Hivi tukiitazama vizuri Meremeta tunaona dalili zozote za usalama wa taifa? Meremeta hii iliyosajiliwa nchini Uingereza, Agosti 1997, na miezi miwili baadaye ikapata Hati ya Kutimiza Masharti hapa nchini, ikawa tawi la kampuni ya nje; hii ndiyo tunaihusisha na usalama wa taifa?
Meremeta hii inayomilikiwa na kampuni ya Triennex (PTY) Ltd ya Afrika Kusini (hisa 50%); Msajili wa Hazina kwa niaba ya Serikali ya Tanzania (hisa 50%); London Law Services Ltd ya Uingereza (hisa 1%) na London Law Secretarial Services Ltd ya Uingereza pia (hisa 1%); ndiyo tunaihusisha na usalama wa taifa? Na asilimia halisi ya hisa za wamiliki ni ipi?
Serikali na Bunge watueleze; usalama wa taifa letu unawekwaje mikononi mwa kampuni za kigeni? Meremeta iliyosajiliwa namna hii, na yenye wamiliki hao waliotajwa, ndiyo tuliyoambiwa na serikali, kwa kinywa cha Waziri wa Nishati na Madini (wakati huo), Nazir Karamagi, kwamba inamilikiwa na serikali yetu kwa asilimia 100?
Na je, Meremeta hii hii ndiyo aliyokuwa akizungumzia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwamba inamilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania?
Tushike lipi, tuache lipi? Nani mwongo nani mkweli? Serikali yetu inataka kuligeuza jeshi letu kuwa dampo la takataka za kifisadi? Hata kama inahusu jeshi, ufisadi huu wa bilioni 155 unamhusu nani katika jeshi au serikali, na unalinda usalama wa taifa gani? Tanzania? Uingereza? Afrika Kusini?
Kina mama wajawazito wanaopoteza uhai; waume zao na watoto wao, wanafaidikaje na bilioni hizi 155 zilizotafunwa na Meremeta? Watoto wetu wanaokosa vitabu, karo, madawati, madarasa, maktaba katika shule za sekondari za kata (na hata nyinginezo), wanafaidikaje na bilioni 155 zilizotafunwa kupitia Meremeta?
Wanajeshi wenyewe tunaowasingizia na kuwafanya mabango ya ufisadi huu, wanafaidikaje (mmoja mmoja au kwa makundi) na bilioni hizi 155 za ufisadi wa Meremeta? Je, serikali inataka kutuambia kwamba hii ndiyo heshima ya jeshi letu?
Au inadhani kwa kuwa wananchi wamejengwa kuogopa jeshi, na kwa kuwa serikali inatumia kigezo cha usalama wa taifa kututisha kujadili suala hili, itafanikiwa kutunyamazisha milele na kutukubalisha kuwa huko kunakofuka moshi huu hakuna moto wowote?
Ni lipi bora kwa usalama wa taifa, serikali kutoa maelezo ya kina na kuwashughulikia wahusika wa ufisadi huo, au kuendelea kulisingizia jeshi letu na kuwatisha wananchi ili wakubwa waendelee kunywa chai ya bilioni 30?
Je, serikali ina uhakika kwamba wanajeshi wetu wanapenda kupewa sifa hii na kutumiwa kama ngao ya wanasiasa kujikingia uchafu wao?
Pale tutakapokuwa sote tumekosa uvumilivu, tuko tayari ‘kupasua matumbo ya vigogo’ hawa ili kuchukua kilicho chetu, serikali itakuwa imebaki na kinga gani, iwapo na wanajeshi wataamua kutetea na kulinda utu na heshima yao?
Leo hii watawatumia wanajeshi kulinda matumbo ya vigogo. Je, itakuwaje kesho wanajeshi wenyewe wakigundua kwamba nao wana matumbo yenye kustahili haki sawa?
Je, vinara wa ari mpya na kasi mpya wako tayari kwa matokeo ya uongo na vitisho vyao? Au wanadhani sisi ambao hatukwenda Ngurdoto hatuna mipango na mikakati ya kujikwamua? Je, kwa utendaji huu wa serikali, taifa letu liko salama?