KAULI tata ya mkongwe wa propaganda za CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru, kwamba waraka uliotolewa na kanisa kuelimisha umma juu ya haki za kiraia na maandalizi ya uchaguzi ‘utaligawa taifa’ na ‘uondolewe’ imenikumbusha kisa cha yeye mwenyewe alivyoigawa CCM miaka minne iliyopita.
Ingawa tayari ameshajibiwa na wasomi na viongozi wenyewe wa dini kwamba angepaswa kuusoma waraka kabla ya kuukosoa, na kwamba kama angekuwa makini angejadili waraka badala ya kuwajadili waliouandika; na ingawa nilishajadili suala hili huko nyuma, nitadokeza upya kipengele kinachomhusu Kingunge, ili kujadili vema hoja yake, na kumsaidia ‘kuzeeka vizuri.’
Ni bahati mbaya kwamba mwaka 2005 baadhi ya viongozi wa kanisa waliposema kwamba mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni chaguo la Mungu, mzee Kingunge, ambaye wakati huo alikuwa bado hajapoteza cheo cha mshauri wa Rais katika masuala ya kisiasa, hakuona kwamba ‘wamechanganya dini na siasa.’
Sababu zinaeleweka. Wakati ule alikuwa mpambe wa mgombea huyohuyo, na alikuwa anamendea ubunge wa kupewa (kuteuliwa) na huyohuyo aliyekuwa amepewa chapa ya ‘chaguo la Mungu.’
Anakumbuka vema, yeye na waliokuwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM wakati wa kujadili na kupunguza idadi ya wagombea ili wabaki watatu wa mwisho (Jakaya Kikwete, Dk. Salim Ahmed Salim na Profesa Mark Mwandosya) kabla ya majina yao kupelekwa mbele ya Mkutano Mkuu.
Baada ya wagombea wote kujieleza na kuomba kura kwa wajumbe, mwenyekiti wa kikao, Rais Benjamin Mkapa, aliwaomba wagombea wote watoke nje, ili kikao kiwajadili.
Kwa mujibu wa taarifa zilizovuja kutoka kwenye kikao hicho, mara baada ya wagombea kutoka nje, mwenyekiti alisema: “Waheshimiwa wajumbe, mnamuonaje Dk. Salim?”
Mmoja baada ya mwingine, walisimama wajumbe kutoka Zanzibar , mithili ya watu walioandaliwa nia moja: kumuonyesha kama mgombea hatari asiyefaa kupewa fursa ya kuwa Rais.
Wakati mashambulizi hayo yakirushwa dhidi ya Dk. Salim, mwenyekiti alikuwa kimya. Baadhi ya wajumbe waliokuwa hawajui kinachoendelea, walipigwa na butwaa, na baadhi yao wakataka kurejesha amani na mwelekeo wa kikao.
Ndipo mjumbe mmoja kutoka mkoa wa Arusha, akanyosha mkono na kuhoji kinachoendelea; na kwamba inakuwaje Dk. Salim anashambuliwa wakati hayupo na hana fursa ya kujitetea dhidi ya tuhuma nzito anazorushiwa.
Kabla mwenyekiti hajajibu hoja ya mjumbe, alisimama mjumbe mwingine, bila hata kunyosha mkono, na bila ruhusa rasmi ya mwenyekiti, akafoka kwa sauti ya amri: “Kaa chini wewe Msomali!” Kimya na mshangao vikatawala; baadaye kikao kikaendelea bila kuwajadili wala kuwashambulia wengine.
Kauli ya mjumbe, mshauri wa rais, mkongwe wa propaganda na fitina za kisiasa, mzee ambaye hataki kuona na kutambua nyakati za mawio ya jua lake kisiasa , ilikuwa hitimisho la mambo mawili.
Kwanza , wajumbe walipata mwelekeo wa hisia za mwenyekiti, kwamba hamtaki Dk. Salim. Pili, kwa kauli za kibaguzi kama hizi, bila kujua, mwenyekiti na watu wake walifanikiwa kukipasua chama, na kupandikiza makundi ya chuki za ndani kwa ndani ambazo zinaendelea kukitafuna chama hadi leo.
Kwa hili, Mzee Kingunge si mwalimu wetu, hasa pale anapotuonya tusisome waraka unaoielimisha jamii juu ya namna ya kuwapata viongozi bora baadaye, na kuwaasa Watanzania wasichague viongozi mafisadi.
Kitendo cha Mzee Kingunge kuibukia Bungeni akawakemea viongozi wa kanisa, kwamba wanachanganya dini na siasa na wanataka kuvuruga jamii, huku akiamuru wafute mwongozo huo unaowapa wananchi elimu ya uraia, ni kielelezo tosha cha uzoefu wake wa propaganda chafu zilizopitwa na wakati, na ambazo zinaendelea kuligawa taifa.
Bahati nzuri ni kwamba Mzee Kingunge ametumbukia katika tafsiri halisi ya alichosema Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam , Method Kilaini, kwamba wanaouogopa waraka wa Kanisa kuhusu elimu hii, ni mafisadi.
Zaidi ya hayo, Mzee Kingunge, licha ya ukurupukaji wake kujadili jambo ambalo hajalisoma vema, amejikuta anaupigia debe waraka huohuo aliotaka kuushambulia.
Katika hili, Watanzania hawako tayari kufokewa na Mzee Kingunge. Lakini swali la msingi kwa Mzee Kingunge ni hili. Kama yeye anadhani viongozi wa dini hawapaswi kujihusisha na siasa za nchi hii, kwa nini yeye mwanasiasa anajihusisha na dini zao?
Au tuseme hivi: kama tafsiri yake ya kutokuchanganya dini na siasa ni viongozi wa dini kutokuzungumzia masuala ya kisiasa, yeye na wanasiasa wengine wanapozungumzia masuala ya dini wanakuwa hawachanganyi siasa za dini? Je, Mzee Kingunge amejielimisha vizuri kuhusu wajibu wa viongozi wa dini kwa jamii? Je, ni vema tukimshtaki yeye kwa kuchanganya siasa na dini?
Nionavyo mimi, ni kwamba baadhi ya wanasiasa na viongozi wa dini hawajajielimisha vema kuhusu dhana hii ya kutokuchanganya dini na siasa. Wamekariri tu kifungu hiki cha maneno, na sasa wanakitumia pale maslahi yao ya kifisadi, ya kisiasa au ya kidini yanapoguswa.
Zaidi ya hayo, Mzee Kingunge amejipa jukumu jipya la kuwa mtetezi wa mafisadi, akidhani ukongwe wake ni kinga tosha ya kuwaepusha wenzake na dhahama ya hasira za umma.
Miaka miwili iliyopita, alijitokeza kuwatetea watuhumiwa wa ufisadi 11 walioorodheshwa na kutanganzwa hadharani. Watu wenye akili waliosikiliza utetezi wake walitema mate chini; kazi ya kuwashughulikia mafisadi ikaendelea, ikiongozwa na wanasiasa wa upinzani.
Leo hii, hata wabunge wenzake wa CCM wanajitapa kuwa wanapambana na ufisadi - ule ule ambao Kingunge alisema haupo. Hata rais (bosi wake) sasa anajitapa kuwa kajiunga na mapambano aliyokuwa anayebeza; anasema anapambana na mafisadi – wale wale waliotetewa na Kingunge.
Katika kuushambulia mwongozo wa kanisa, Mzee Kingunge amekosa busara ndogo tu ya kuonyesha vifungu vya mwongozo huo ambavyo vinatishia amani na umoja wa kitaifa, kiasi cha kuelekea ‘kuligawa taifa’ na kuleta ‘machafuko’ kama anavyodai yeye.
Maana, kama ni kuligawa taifa, CCM imeshaligawa siku nyingi. Na kama ukongwe wa Mzee Kingunge unaosifiwa ndani ya CCM haumsaidii kulitambua hili, ni wazi kwamba hata huo ubunge aliopewa haulisaidii taifa wala chama na serikali iliyomteua.
Analopasa kujua ni kwamba vita dhidi ya ufisadi ni jitihada za wananchi (wa imani, makabila na tofauti zote) kurejesha uadilifu, uhai na umoja wa kitaifa. Kuthubutu kuwanyamazisha hawa, ni jitihada chafu zinazostahili kusimamiwa, kutetewa na kufanywa na Ibilisi wa kisiasa.
Mzee Kingunge na wenzake wanaofikiri kama yeye, wanaotaka kulinyamazisha kanisa lisikemee mafisadi au lisielimishe wananchi kuhusu haki zao za kiraia, wanapaswa wajielimishe zaidi kuhusu dhana hii ya kutenganisha dini na siasa.
Wajue kuwa kutenganisha dini na siasa hakuna maana kwamba wananchi wenye dini zao wasiwe viongozi au wanachama wa vyama vya siasa au wanaharakati na wahamasishaji wa masuala ya maendeleo ya nchi. Wala haina maana kwamba viongozi wa dini hawana jukumu la kuwashauri wananchi juu ya mwenendo wa kisiasa nchini.
Ndiyo maana wananchi hao hao wenye dini, tena wengine ni viongozi wa dini, wanapewa nafasi za uongozi wa kisiasa na kijamii. Ndiyo maana wanashiriki kampeni na kupiga kura.
Kinachokataliwa na kusisitizwa katika dhana ya kutenganisha dini na siasa ni kimoja: dini za watu, zisiwe dini za taifa.
Na huu ndiyo msingi uliokusudiwa na waasisi wa dhana hii, kwamba taasisi za kidini na za kiserikali (kidola) zitenganishwe. Kimsingi, dhana hii ni zuio la kimantiki, kisheria na kisiasa dhidi ya serikali ili isiingilie na kutawala imani au dini za raia wake; kila raia awe na uhuru wa kuabudu kadiri ya imani yake; yaani kusiwepo na imani yoyote ambayo ndiyo dini rasmi ya taifa.
Wasomaji wa historia (ambayo Mzee Kingunge alipaswa kuijua) wanafahamu kuwa huko tulikotoka, katika mataifa makubwa yaliyotutangulia, viongozi wa kidini waliwahi kupatikana kwa kuteuliwa na wanasiasa (wafalme na malkia); na katika nyakati fulani viongozi wa dini ndiyo waliongoza dola kisiasa.
Historia imejaa orodha ya wafalme wa awali wa Kirumi (hadi mwaka 300 BK) waliojipa vyeo vya juu vya kidini, na wengine walifikia mahali pa kutaka waabudiwe kama miungu hata baada ya vifo vyao.
Wayahudi na Wakristo ndiyo makundi ya awali yaliyopambana na changamoto hii ya kisiasa; wakakubali kuyatambua mamlaka ya kisiasa ya watawala, lakini wakakataa kufuata dini rasmi ya watawala hao; wakaitwa waasi na maadui wa dola, na baadhi yao walipoteza maisha.
Hata katika nchi za Ulaya Magharibi, kwenye zama za kati, mapambano ya wafuasi wa dini kujinasua kutoka kwenye makucha ya watawala, na baadaye jitihada za wanaharakati kujinasua katika mwingiliano wa nguvu za kidini kuhusu masuala ya kiroho na ya kimwili, uliozifanya dini kadhaa ziwe ndizo rasmi za kufuatwa na raia wote, yakifuatwa na kuchochewa na andiko la Martini Luther juu ya ‘falme mbili,’ ndiyo asili ya harakati za kutenganisha dini na siasa.
Dosari ya harakati hizi ilijitokeza katika miaka ya 1530, baada ya Mfalme Henry VIII wa Uingereza, kujitenga na Kanisa Katoliki akaanzisha Kanisa la Uingereza (Anglikana) ambalo lilisukwa tena kwenye siasa, na kuufanya Uanglikana kuwa dini rasmi ya taifa Uingereza.
Hiki ndicho tunachokikataa Tanzania ; kwamba hatuna dini rasmi ya taifa, na kwa kuzingatia mantiki ya Mwanafalsafa Muingereza John Locke, tunasisitiza kwamba imani ya mtu iongozwe na dhamiri yake, na uhuru wake wa kuchagua ibada anayoitaka.
Serikali haina mamlaka ya kutawala dhamiri zetu wala kutuchagulia imani za kufuata, na jinsi ya kuzifuata. Ndiyo maana ya serikali kutokuwa na dini. Ndiyo asili ya uvumilivu wa kidini katika jamii yenye waamini wa dini mbalimbali. Ndiyo tafsiri ya kutenganisha dini na siasa.
Lakini majukumu ya dola na dini yanabaki pale pale. Taasisi moja inajishughulisha na masuala ya kimwili, ya muda, yapitayo haraka; nyingine inajishughulisha na masuala ya kiroho, yadumuyo, yanayotafuta na kufafanua uhusiano wa roho na mwili, viumbe na muumba.
Kama wasemavyo baadhi ya wanzuoni, mataifa na serikali huja na kupita; lakini dini hudumu. Jukumu kuu la dini ni kusimika, kukoleza na kutetea misingi ya kimaadili.
Ni jukumu la dini kujenga na kuboresha mustakabali wa kijamii kwa kutetea misingi hii ya kimaadili, kulinda heshima na utu wa binadamu, hata kama itawalazimu watetezi kutofautiana na watawala. Hatuwezi kuwa na misingi ya kimaadili bila kutambua na kutetea utu wa binadamu huyu huyu.
Kwa hiyo, kazi ya dini ni kupinga mifumo yoyote inayomdhulumu binadamu haki, heshima na utu wake katika jamii; iwe katika elimu, uchumi, siasa na kadhalika.
Hapa ndipo dini zinapata nguvu na mamlaka ya kukemea uovu bila kutazama sura za wanaotenda uovu huo. Mzee Kingunge anaogopa kwa kuwa kemeo la viongozi wa dini linamnyima usingizi. Anaogopa elimu inayotolewa itawaamsha wananchi kujua uovu unaotendwana watawala na wanasiasa wasio makini.
Asichotaka kujua, na asichoweza kuzuia ni kwamba taasisi za dini zimeshiriki na zitaendelea vema, kama mwalimu, katika kufafanua na kukuza tunu mbalimbali za kijamii, kwa njia mbalimbali.
Na mwongozo huu wa kanisa unalenga katika kudhibiti kasi ya ufisadi unaosambazwa na Ibilisi wa kisiasa wanaojificha nyuma ya propaganda za Mzee Kingunge. Kwa mara nyingine, Kingunge anathubutu kutugawa; na tumekataa kumsikiliza.